Kenya imeamua kufunga mpaka wake na Ethiopia kwa muda usiojulikana kufuatia mapigano yanayoendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo jirani ambayo yamezua wasiwasi kieneo na kimataifa.

Mbali na tangazo hilo kufunga mpaka wake na Ethiopia, serikali ya Kenya imetangaza pia kuwa, imezidisha doria kwenye mpaka wa kilomita 800 ili kudhibiti kuingia nchini kwa wahamiaji haramu.

Serikali ya Nairobi imetawaka pia Wakenya kuwa waangalifu zaidi hasa wale wanaoishi katika maeneo yaliyo jirani na mpaka wa nchi mbili hizo.

Hayo yanajiri wakati Baraza la Bawaziri la Ethiopia limetangaza hali ya hatari nchini kote kwa muda wa miezi sita ijayo kufuatia waasi wa Tigray kuelekea mji mkuu Addis Ababa.

Waziri Mkuu wa nchi hiyo Abiy Ahmed alitangaza hali ya hatari katika kukabiliana na kile alichokiita tishio ambalo linaweza kuisukuma nchi hiyo kusambaratika.

Kundi la Oromo ambalo linashirikiana na waasi wa Tigray nchini Ethiopia limesema kuwa, mji mkuu Addis Ababa huenda ukadhibitiwa katika miezi au wiki kadhaa zijazo, wakati wapiganaji wakisonga mbele kuelekea kusini mwa nchi. Jeshi la Ukombozi wa Watu wa Tigray - TPLF, ambalo limekuwa likipigana na serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kwa mwaka mmoja sasa, limedai kudhibiti maeneo muhimu katika siku za karibuni.

Katika upande mwingine, Michelle Bachelet Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani ukatili na unayanyasi unaoripotiwa kufanyika katika jimbo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia na kuzihimiza pande zote kuitikia wito wa kimataifa wa kukomesha vitendo hivyo