Utumwa wa mapenzi ni hali ya kuwa/kuishi na mpenzi ambaye humpendi kwa moyo wako lakini unalazimika kuwa naye kwa sababu binafsi. 

Maana ya pili ni kuwa/kuishi na mpenzi ambaye hakupendi na unajua kabisa hana mapenzi na wewe lakini unalazimisha ukiamini kwamba siku moja anaweza kubadili uamuzi wake.

Aina hizi mbili za utumwa ndizo zinazowasumbua wengi na kuendelea kuteseka katika uhusiano ambao mwisho wake ni matatizo.

Wakati unafanya hayo, unatakiwa ukumbuke jambo moja muhimu; wewe ni mtu mzima na unaendelea kukua, umri unasogea hivyo kuendelea kung’ang’ania penzi la mtu ambaye hana mwelekeo (kwa namna moja kati ya mbili nilizoainisha hapo juu) unajiweka katika nafasi ya kutoingia kwenye ndoa.

Uhusiano bila penzi la kweli
Uhusiano wa aina hii ni ule ambao mmoja wao anakuwa hana mapenzi kwa mwezake lakini analazimisha kuwa naye kwa sababu ya kupata masilahi. Mapenzi ya aina hii siku hizi yameenea sana.

Unakuta mwanamke anaamua kuwa na mwanaume fulani ingawa anajua wazi kwamba hampendi lakini kwa sababu jamaa kashaonyesha mapenzi kwake na anajua wazi anampenda, basi anakubali kwa sababu ya kupata kitu.

Tatizo linakuja pale ambapo jamaa anaamua kufunga naye ndoa moja kwa moja, mara nyingi kwanza huanza kusita lakini baada ya kufikiria kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kupata ushauri kwa marafiki (wenye tamaa kama yeye) huamua kuingia katika ndoa na mwanaume ambaye hajampenda akitegemea kupata maisha mazuri.