Jeshi la Uganda limeanzisha mashambulizi ya pamoja ya anga na ardhini dhidi ya kundi la waasi la Allied Democratic Forces -ADF, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Msemaji wa Jeshi la Wananchi wa Uganda Brigedia Jenerali Flavia Byekwaso amethibitisha hayo kupitia akaunti yake rasmi ya twitter.

Alisema kuwa operesheni hizo zilifanywa na washirika wa Congo, dhidi ya kambi za ADF, lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu maeneo ambayo mashambulizi hayo yamefanywa.

Mamlaka ya Uganda inalaumu ADF, ambayo inashirikiana na Islamic State (IS) kwa msururu wa mashambulizi ya mabomu nchini humo tangu Oktoba.

Wiki mbili zilizopita, IS ilidai kuhusika na milipuko miwili ya mabomu nje kidogo ya Kituo Kikuu cha Polisi cha Kampala na karibu na Bunge.

Takriban watu watano wameuawa katika milipuko hii ya mabomu, baadhi ya mashambulizi yakiwa ya kujitoa mhanga, kwa mujibu wa Polisi wa Uganda.