Na WAMJW-DSM
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wataalam wa Afya kuelimisha Jamii kuhusu Usonji na kuiwezesha kupata uelewa na kuondoa unyanyapaa kwa wenye changamoto hiyo.

Dkt. Gwajima amesema hayo Jijini DSM wakati akifungua hafla ya uelimishaji jamii kuhusu Usonji, sambamba na uchangishaji fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana wenye usonji kupata mafunzo ya kilimo mahiri yaliyoandaliwa na Lukiza Autism Foundation.

“Nitoe rai kwa wataalam wetu wa afya na elimu, madaktari, Ustawi wa jamii, walimu wa watoto wenye uhitaji maalum, waandishi wa habari na wengine wote mlioshiriki katika hafla hii, kutumia elimu na uelewa uliopatikana leo kuwaelimisha wengine” Amesema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima amesema Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2020 zinaonesha kuwa katika kila watoto 132 Duniani, mtoto mmoja ana Usonji.

“Hapa Tanzania,takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kuwa, wanafunzi 1416 katika shule 18 za Msingi waliofanyiwa usahili, wana usonji.” Alisema Dkt. GWAJIMA

Katika hatua nyingine, Dkt Gwajima amewataka washiriki wa hafla hiyo kuzingatia kuyafanyia kazi mapendekezo ya washiriki ili kujenga upendo na kuondoa unyanyapaa katika Jamii.

Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kufanya tafiti kuhusu tatizo la usonji, na kuweka wazi kuwa, Serikali itatoa ushirikiano kuhakikisha kuwa tafiti hizi zinafanyika na matokeo ya tafiti hizo yanatumika kuimarisha huduma kwa watoto wenye Usonji nchini.

“Ninatoa wito na kuhimiza Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kufanya tafiti kuhusu tatizo la usonji na serikali itatoa ushirikiano kuhakikisha kuwa tafiti hizi zinafanyika na matokeo ya tafiti hizo yanatumika kuimarisha huduma kwa watoto wenye Usonji”, amesisitiza Waziri Gwajima.