Kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, imeanza kusikilizwa, Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ndogo imeanza kusikilizwa mahakamani hapo mbele ya Jaji Joackim Tiganga, leo Jumatano, tarehe 10 Novemba 2021.
Kesi hiyo inatokana na mapingamizi ya upande wa utetezi dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya, wakiiomba mahakama hiyo isiyapokee kwa madai kuwa si halali kisheria.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, ameieleza mahakama hiyo kuwa wanapanga kuita mashahidi sita na vielelezo vinne.
Wakili Kidando ameileza mahakama hiyo kuwa, leo wana shahidi mmoja ambaye ameanza kutoa ushahidi wake, mahakamani hapo.
Shahidi huyo ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wilayani Arumeru, SP Jumanne Malangahe, ameanza kutoa ushahidi wake akiongozwa na Wakili Kidando.
Mapingamizi hayo yaliibuka baada ya shahidi wa nane wa jamhuri, Jumanne Malangahe, kuiomba mahakama hiyo iipokee nyaraka ya maelezo hayo, kama sehemu ya ushahidi wa upande wa mashtaka.
Katika hoja za upande wa utetezi, walidai Ling’wenya hakuwahi kuchukuliwa maelezo hayo, kama ilivyodaiwa na SP Jumanne, kwamba aliyachukua baada ya kumhoji tarehe 7 Agosti 2020, Katika Kituo cha Polisi cha Kati Dar es Salaam.
Mawakili wa utetezi walidai kuwa, Ling’wenya alilalizimishwa kusaini nyaraka ya maelezo hayo kwa kupewa mateso ya kisaikolojia. Na kwamba hakuisoma kujua kilichomo ndani yake.