BAADA ya kuwa mbishi kwa miaka mingi, hatimaye rapa maarufu kutoka pande za MarekaniJay Z amejiunga na familia ya watumiaji wa mtandao wa Instagram Duniani na kujizolea wafuasi (followers) zaidi ya milioni moja ndani ya saa tatu tu tangu ajiunge.

Kwenye akaunti yake hiyo amemfuata mtu mmoja pekee ambaye ni mke wake mwanamuziki maarufu Duniani Beyoncé Giselle Knowles-Carter.

Uamuzi huo wa Jay Z kujiunga kwenye mtandao huo mkubwa duniani kunajibu maswali ya mashabiki wa rapa huyo ambao wengi walikuwa wakihoji sababu ya yeye kuamua kuupotezea kwa miaka mingi mtandao huo, licha ya kundi kubwa la wasanii na wajasiriamali ulimwenguni kutumia Instagram kukuza biashara zao, brand zao na kukutana na watu wa matabaka mbalimbali.

Inaweza kuwa Jay z alikuwa akiichukia sana mitandao ya kijamii. Hili linakuja kufuatia maneno aliyowahi kuyazungumza rapa mwenzake, Meek Mill kuhusu alichowahi kuambiwa na Jay Z siku za nyuma.

“Jayz aliwahi kuniambia kuwa ulimwengu huu wa mitandao ya kijamii uliundwa kwa ajili ya watu ambao hata hawawezi kuzungumza kama hawakuwepo,” aliwahi kuandika Meek Mill.

Jay Z alijiunga na Instagram kwa mara ya kwanza Agosti 29, 2015, na kupost kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa marehemu Michael Jackson, lakini akaifuta programu hiyo masaa 14 tu baada ya kupata wafuasi 100,000 kwenye mtandao huo.