Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi jijini Dar es Salaam, imekataa kupokea kitabu cha kumbumbuku za mahabusu, chenye taarifa zinazodai Mohammed Ling’wenya, aliwekwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.
Ling’wenya ni mshtakiwa wa tatu katika kesi yenye mashtaka ya kupanga vitendo vya kigaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, akiwemo Ling’wenya. Wengine ni; Halfan Hassan Bwire na Adam Kasekwa.
Kitabu hiko ambacho shahidi upande wa mashtaka, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Arumeru, SP Jumanne Malangahe, aliiomba mahakama hiyo ikipokee kwa ajili ya utambuzi, kimekataliwa leo Alhamisi, tarehe 11 Novemba 2021.
Uamuzi huo, umetolewa na Jaji Joackim Tiganga, katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, inayowakabili Mbowe na wenzake ya kupanga njama za vitendo vya kigaidi.
Pingamizi hilo liliibuliwa na mawakili wa utetezi, wakiiomba mahakama hiyo isipokee kitabu hicho, kwa ajili ya utambuzi, kama ilivyoombwa SP Jumanne, wakidai shahidi aliyekileta kitabu hicho hakuweka msingi wa kuonesha kuaminika kwake pamoja na nyaraka hiyo.
Na wala hakuonesha mlolongo wa utunzaji kitabu hicho (Chain of Custody), kutoka mahakamani hapo hadi kumfikia yeye.
Akitoa uamuzi mdogo wa pingamizi hilo, Jaji Tiganga amesema mahakama hiyo inakataa kukipokea kielelezo hiko kwa ajili ya utambuzi, kwa kuwa shahidi ameshindwa kuonesha mlolongo wa utunzwaji wake.
“Mahakama inaona ili kuthibitisha kilelezo kimefika kihalali kwa shahidi lazima ionekana kimeombwa au kufuata utaratibu wa kupelekwa kwa shahidi na kuonekana kimeingia kwenye mkono wake.
“Lakini kinajikuta kimefikia kwa shahidi bila kuonesha kimemfikia namna gani. Mahakama inaonesha hauko ushahidi wa kutosha kuonesha kilelezo hiko kimemfikiaje,” amesema Jaji Tiganga.
Jaji Tiganga amesema; “hakuna ushahidi ulioonesha kiliombwa kwa mtunza vilelezo wa mahakama au alikitoa kwa upande wa mashtaka au shahidi ili kuonesha mtiririko wa Chain of Custody, shahidi anaonekana ameshindwa kutengeneza chain of custody, kwa sababu hiyo mahakama inakataa kupokea kilelezo hiki.”
Kufuatia uamuzi huo, Jaji Tiganga alielekeza shahidi huyo aendelee kutoa ushahidi wake aliouanza jana Jumatano katika kesi hiyo ndogo.