Na. WAMJW- DODOMA
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, JInsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi, amezidi kuhimiza matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Serikali kwenye Wizara,hospitali na taasisi zake, kuweka mpango utakao kuja na matokeo chanya na ambao hautakuwa na matumizi ambayo hayakuelekezwa na Serikali katika fedha za Uviko-19.

Prof. Makubi amesema hayo  Novemba, 03, 2021. wakati akifungua kikao kazi cha Wakurugenzi wa Taasisi, hospitali za Taifa Maalumu za Kanda, Rufaa za Mikoa pamoja na Waganga Wakuu wa Mikoa kilichofanyika jijini Dodoma.

Kikao kazi kilichokua na lengo la kuelekezana namna ya utekelezaji wa Mpango wa Mradi wa Afya kwa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano ya UVIKO-19 ambapo Wizara ya Afya imepokea bilioni 259.2 na kuzisimamia mradi huo pamoja na Taasisi na hospitali zake zilizo chini yake.

Amesema kuwa fedha hizo zimeelekezwa kwenye huduma za dharura, Wagonjwa mahututi, huduma za kimaabara, masuala ya Mtandao sambamba na kuimarisha huduma kwenye Hospitali za kanda na za Rufaa za Mikoa, Pamoja na eneo la tafiti.

“Mhe. Dorothy Gwajima, Waziri wetu, amekuwa mstari wa mbele, kuhimiza matumizi sahihi ya fedha hizi za Uviko-19, hivyo tumpongeze sana Mhe. Waziri kwa jinsi anavyosimamia kwa umahiri na weledi na jinsi anavyotoa maelekezo kwetu sisi wasaidizi wake ili kuona tunafikia malengo tuliyojiwekea” amesema Prof. Makubi

Prof. Makubi amesema, ili waweze kwenda vizuri na kufikia malengo katika matumizi ya fedha hizo, lazima kuzingatia uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja. “Kipaumbele katika matumizi ya fedha hizi ni Thamani ya fedha kwa miradi mtakayotekeleza kwenye maeneo yenu, mzingatie sheria ya manunuzi kwenye kila hatua, shirikisheni menejimenti ndani ya taasisi zenu lakini pia wewe Mkurugenzi ujue kinacho endelea kwenye Mkoa wako au taasisi yako. Amesema Prof. Makubi.

Katibu Mkuu Prof. Makubi, amewataka kuzingatia Ubora wa vifaa kwa bajeti ambayo imetolewa kwao, kama maelekezo ya Mhe. Rais yalivyotaka, vilevile kuzingatiwa kwa kanuni za manunuzi hasa kwa kutumia Mzabuni mmoja kutokana na muda wa matumizi ya fedha hizo kuwa mfupi,  “tumieni uzoefu mlionao, kati ya wazabuni wengi ambao tayari mlisha wahi kufanya nao kazi chagueni wenye ufanisi miongoni mwao” alisema Prof. Makubi.

Prof. Makubi ametaka kushirikishwa kwa Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya sambamba na Viongozi wengine walipo katika maeno yao, pamoja na wananchi ili wawe na uelewa wa pamoja wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo na kuleta dhana ya umiliki wa miradi kwa kila mwananchi.

Katika hatua nyingine Prof. Makubi, amewakumbusha viongozi hao, kushiriki ipasavyo katika mpango wa pili wa kampeni ya Uviko-19, hasa wakati huu ambao viashiria vya wimbi la nne limeanza kujitokeza.

“Tulifanya kazi vizuri sana baada ya uzinduzi wa Mpango Shirikishi na harakishi wa awamu ya kwanza, ni rai yangu sasa, kwakua tarehe 03 Novemba, 2021, tulizindua mpango wa awamu ya pili, kila mmoja kwa wetu awe mstari wa mbele kuhakikisha afua ya chanjo ambayo tumeichagua kama njia mbadala yakupungua maumivu kwa mtu anayepata Ugonjwa wa Uviko-19 basi tukazidi kuhamasisha na kushawishi watu waendelee kuchanja kwa wingi” amesema Prof. Makubi.

Takwimu zinaonesha hadi kufikia sasa zaidi ya watu Milioni 1.1 tayari wamepatiwa chanjo ya uviko-19, ambapo amesema ni vizuri tukaongeza kasi ya kampeni ili watu wengi zaidi waweze kuchanjwa kwenye ngazi za Mitaa na Vijiji, huku akitaka kuungwa mkono awamu ya pili, ilitufikie adhma yakuchanja angalau watu 80,000 hadi 100,000 kwa siku.

Ameonya kuwa wasipofanya hivyo itachukua miaka mingi kufikia watu Mil.35 ambao ndio asilimia 60 ya wananchi ambao wakishachanja ndio tutakuwa tumejenga kinga ya mwili ya mtu mmoja mmoja.