Na. WAMJW – Dar es Salaam
Wafamasia nchini wametakiwa kusimamia miiko na maadili ya taaluma yao katika vituo vyao vya kazi na kuepuka vitendo viovu ikiwemo wizi wa dawa na ulaji rushwa.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa Brig. Jen. Dkt. Gabriel Sauli Mhidize, alipo muwakilishai, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel Katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Fundi Dawa Sanifu na Fundi Dawa Wasaidizi (TAPHATA) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mhidize kupitia ujumbe wa Naibu waziri wa Afya amesema, mkutano huo wa wana taaluma wote wa famasia wanatakuwa kuyafanyia kazi yote watakayo jifunza.
“Naamini mtaenda kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi katika kufikia lengo la utoaji wa huduma bora za Afya nchini” amesema Dkt. Mhidize
Kwa upande wake Msajili Baraza la Famasi, Elizabeth Shekalaghe ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya iweke miongozo itakayotoa maelekezo kwenye sekta zote (binafsi na Serikali) kuwa na Wataalamu sahihi wa dawa katika ngazi za zahanati, vituo vya Afya na Hospitalini.
Bi.Shekalaghe amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza Ajira kwa kada za wafamasia na zitasaidia kuboresha utoaji sahihi wa huduma bora za Afya nchini.
“Tukiwa tunaenda kwenye uchumi wa viwanda kwa kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, tunaomba viwanda vilivyopo nchini kuajili Wataalamu sahihi ili kuboresha uzalishaji wa dawa”amesema Shekalaghe.
Aidha, Bi.Shekalaghe ameiomba Wizara ya Afya kupitia taasisi zake kupitia upya viwango vya madaraja ya ufaulu wa kujiunga na vyuo vinavyotoa kozi ya Fundi Dawa Sanifu na Fundi Dawa Wasaidizi ili kupata Wataalamu sahihi na wenye uwezo wa kutoa huduma.
Mkutano huo utadumu kwa siku mbili kuanzia 29-30 mwezi wa 11, 2021 na umewashirikisha Wana taaluma wa ufamasia kutoka Tanzania Bara.