Rais wa China Xi Jinping amefanya mkutano na mwenzake wa Marekani rais Joe Biden kuonya kuwa kuhimiza uhuru wa Taiwan kutakuwa ni sawa na "kuchezea moto".

Mazungumzo hayo yanachukuliwa kuwa muhimu zaidi tangu Bw Biden aingie madarakani mwezi Januari.

Pande zote mbili zimesisitiza uhusiano wa kibinafsi wa viongozi hao wawili na mkutano huo ulikuwa ni jaribio la kupunguza mvutano.

Lakini hawakuweza kuepuka kuzungumzia mada moja tata zaidi ya kujitawala kwa kisiwa cha Taiwan.

China inaiona Taiwan kama jimbo lililojitenga na siku moja linaweza kuunganishwa tena na bara.

Marekani inatambua kuwa ina uhusiano rasmi na China. Lakini pia imeahidi kuisaidia Taiwan kujilinda endapo litatokea shambulizi.

Gazeti la serikali ya China Global Times lilisema Bw Xi alilaumu mvutano wa hivi karibuni kutokana na "majaribio ya mara kwa mara ya mamlaka ya Taiwan kutafuta uungwaji mkono wa Marekani kwa ajenda yao ya uhuru pamoja na nia ya baadhi ya Wamarekani kutumia Taiwan kuidhibiti China".

"Hatua kama hizo ni hatari sana, kama vile kucheza na moto. Yeyote anayecheza na moto atateketea," ilisema.

Credit:BBC