Raia wa Austria ambao hawajapatiwa chanjo dhidi ya virusi vya corona, watashindwa kutoka nje kuanzia usiku wa leo baada ya serikali kutangaza marufuku hiyo ili kudhibiti kasi ya maambukizi.

Marufuku hiyo inawahusu watu wasiochanjwa wenye umri wa kuanzia miaka 12 kutembea nje usiku, isipokuwa kwa shughuli za kimsingi kama vile kazi, manunuzi ya vyakula au kupata chanjo.

Serikali ina wasiwasi kwamba huenda wahudumu wa hospitali wataelemewa na wimbi la ongezeko la wagonjwa wa Covid-19. 

Marufuku hiyo itaawaathiri watu milioni 2 katika taifa hilo lenye jumla ya watu milioni 8.9.Austria ni moja kati ya mataifa yenye idadi ndogo ya watu waliochanjwa barani Ulaya. 

Ni asilimi 65 tu ya idadi jumla ya raia ambao wamepatiwa chanjo ya corona. Hali imezidi kuwa ya wasiwasi kutokana na kuongezeka kwa maambukizi katika siku za hivi karibuni.