Na. Edward Kondela
Serikali imewataka maafisa wafawidhi waliopo katika vituo vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria, kuhakikisha wanadhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nchi za jirani pamoja na kuzuia uvuvi haramu.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema hayo jana(28.10.2021) katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Mtumba jijini Dodoma, wakati akikabidhi injini za kupachika kwenye boti zenye uwezo “HP 40” kwa vituo vitano vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi Kanda ya Ziwa Victoria.

 “Ni matumaini yangu kuwa injini hizi zitakuwa chachu kwa vituo hivi kufanya kazi kwa weledi pamoja na kusimamia ulinzi wa rasilimali za uvuvi.” Amesema Dkt. Tamatamah

Aidha, amesema ili kufikia malengo ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kukusanya maduhuli ya Shilingi Bilioni 40 kwa mwaka wa fedha 2021/22, injini hizo zitumike katika kuhakikisha vituo husika vinakusanya maduhuli ili kufikia malengo waliyojiwekea na kufikia malengo makuu ya wizara.

 Nao baadhi ya maafisa wafawidhi waliokabidhiwa injini za boti kwa ajili ya vituo vyao vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi wamesema injini hizo zitasaidia kuongeza nguvu katika kudhibiti uvuvi haramu.

Wameongeza pia injini hizo zitasaidia katika kufuatilia ukusanyaji wa mapato ambayo ni moja ya mikakati ya wizara na kudhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi kwenda nchi za jirani.

 Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Idara ya Uvuvi imenunua injini sita za kupachika kwenye boti zenye thamani ya Shilingi Milioni 68.1 kwa ajili ya kuimarisha Sekta ya Uvuvi nchini.

Vituo vitano vya ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi vilivyokabidhiwa injini hizo ni Kanda ya Simiyu na Magu, Kanda ya Mwanza, Kanda ya Ukerewe, Kanda ya Geita na Kanda ya Marehe Mkoani Kagera.