Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ametoa ufafanuzi wa jinsi Wizara ya Maliasili na Utalii itakavyozitumia shilingi Bil. 90.2 ilizopewa kutoka kwenye fungu la fedha za mapambano ya UVIKO 19  ya Shilingi trilion 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) kuwa  sehemu kubwa fedha hizo  zitatumika kwa ajili ya kununulia vifaa vya kupimia ugonjwa wa UVIKO 19 pamoja na kuboresha miundombinu katika maeneo ya Hifadhi.

Aidha, Dkt.Ndumbaro amesema fedha hiyo  itatumika pia kwa ajili ya kugharamia kutoa mafunzo kwa wadau wa utalii wakiwemo madereva wa magari ya watalii, waongoza watalii, wabeba mizigo pamoja na wahudumu wa hoteli  za kitalii,

Ameyasema hayo leo Jijini Arusha  wakati wa mkutano wa Wizara ya Maliasili na Utalii na  Sekta binafsi ( TPSF) uliolenga kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazokabili sekta ya utalii nchini hususani katika kipindi cha UVIKO 19

Katika mkutano huo wadau mbalimbali  wa Utalii wameshiriki katika mkutano huo wakiwemo Chama cha Waongoza Watalii (TATO), Baraza la Biashara la Taifa, Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Chama cha Waongoza Watalii, Chama cha  wadau wa Utalii wa Utamaduni (TACTO) pamoja na Chama cha Mahoteli a Tanzania (HAT)

Waziri Dkt.Ndumbaro amesema Mhe.Rais Samia Suluhu  Hassan ametoa fedha hizo ili ziweze kuinyanyua sekta ya utalii nchini kufuatia janga la UVIKO 19 ambalo limeiacha sekta ya utalii katika hali tete huku watalii wakisitisha safari kuja nchini kwa ajili ya ugonjwa huo

Amefafanua kuwa vifaa vitakavyonunuliwa kwa ajili ya vifaa vya kupimia UVIKO 19  vitasambazwa maeneo yote ya vivutio vya utalii ili kuwasaidia watalii pindi watakapopimwa  wapewe majibu yao huko huko tofauti na ilivyo sasa

" Tumedhamiria kuondoa usumbufu ili watalii watakapokuja nchini wasiweze kupata usumbufu kwa kuhakikisha kila hifadhi inaweza kutoa huduma hizo kwa haraka ili kuwafanya watalii wasikae kusubiri matokeo kwa muda mrefu " alisisitiza Dkt.Ndumbaro

Akizungumzia kuhusiana na miundombinu, Dkt.Ndumbaro amesema ujio wa fedha hizo zitasaidia kufungua Hifadhi kama vile Hifadhi ya Taifa ya Nyerere imekuwa na barabara nyingi lakini barabara hizo zimekuwa hazipitiki hivyo fedha hizo zitaboresha barabara ili ziweze kupitika mwaka mzima

Mbali na hiyo, Dkt. Ndumbaro amesema barabara zitaboreshwa huku  barabara nyingine zikifunguliwa katika maeneo ya Hifadhi ambazo hazina miundombinu hiyo  ili maeneo hayo yaweze kufikika

" Barabara ikiwa nzuri na wewe una hoteli yako  ipo ndani sana Watalii watakuja kulala katika hoteli yako kwa sababu kuna barabara nzuri, hivyo hela hii inakwenda kufanya kazi hiyo" amesema Dkt.Ndumbaro

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi ( TPSF)  Angelina Ngalula amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kujitoa kuisaidia sekta ya Utalii nchini ''Tunaomba salamu zifike kwa Mhe. Rais kwa juhudi za kuendeleza utalii kwa kututafutia fedha kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF)


" Tumemuona anavyoipambania sekta ya utalii kupitia kipindi chake maarufu alichokiasisi cha Royal Tour ambacho kimeongeza ujasiri kwa Wawekezaji wa sekta ya utalii nchini, tunampongeza sana Rais wetu" alisema Mwenyekiti wa TPSF, Ngalula

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula amewataka wadau wa utalii nchini kuungana kuwa kitu kimoja ili wanapotaka kuweza kuwasilisha agenda zao Serikalini ziweze kukubaliwa na kufanyiwa kazi ,

Awali, Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara,  Dkt.Godwill Wanga aliiomba Wizara kupitia fedha zilizotolewa na IMF za kupambana na UVIKO 19 ili.ziweze kusaidia kuboresha miundombinu zikiwemo barabara  pamoja na viwanja vya ndege ili kuwavutia watalii wanapotembelea vivutio vya utalii waweze kusafiri kiurahisi

Aidha, Dkt. Wanga aliiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia fedha hizo kusaidia kutoa mafunzo kwa wadau wa utalii ili kuwawezesha kutoa huduma bora kwa watalii nchini ombi ambalo limekubaliwa na litaanza kufanyiwa kazi