Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma nchini kuwa wanyenyekevu wanapotoa huduma kwa wananchi ili wawe na imani na Serikali yao.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Umma wa Mkoa wa Mara wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.  

Mhe. Mchengerwa amesema Watumishi wa Umma hawana budi kuwatumikia wananchi kwa unyenyekevu, uadilifu na moyo wa upendo kwani wameajiriwa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

“Fanyeni kazi kwa uadilifu, kazi tunazozifanya ni kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, tumeajiriwa na wananchi, nchi hii ni ya wananachi, tujishushe kwa wananchi, tutekeleze majukumu yetu, tujenge matumaini kwa wananchi, tuwatembelee kusikiliza changamoto zao kwani tusipofanya hivyo tutakuwa hatuwatendei haki,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Ameongeza kuwa, hakuna atakayedumu katika kazi kwani kila mmoja anapita, hivyo ni vema tufanye kazi zetu kama ibada hasa katika kuwahudumia wananchi ili hata ukiondoka kwenye nafasi yako ukumbukwe kwa mema.

Amewasihi watumishi wanapotekeleza majukumu yao kushirikiana na wananchi hasa katika kutoa taarifa ya miradi mbalimbali inayotekelezwa ili wajue ni nini kinaendelea katika maeneo yao.

Mhe. Mchengerwa amesema, Serikali inatamua haki za wananchi hivyo watumishi wa umma tufanye kazi kwa bidii na uadilifu ikiwemo kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhakikisha fedha za miradi zinazotolewa zinafanya kazi iliyokusudiwa.

Mhe. Mchengerwa ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan inatekeleza miradi mingi ya maendeleo na kutoa mfano wa madarasa 15,000 ambayo Serikali inaenda kuyajenga hivyo amewasisitiza Watumishi kusimamia kikamilifu fedha zitakazotolewa, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.