Waziri wa Nishati, Mh. January Yusuf Makamba, Oktoba 18, 2021 kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi wa mataifa ya Saudi Arabia, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Algeria nchini Tanzania, kwenye ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Waziri Makamba, mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha uhusiano wa kisekta baina ya Tanzania na nchi hizo, ili kuiongezea tija sekta ya nishati kwa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji.

“Rais wetu Mh. Samia Suluhu Hassan yuko mstari wa mbele katika kuhakikisha sekta ya nishati inaimarika na kulinufaisha taifa kiuchumi, hususani katika kuvutia wawekezaji na kutumia vyema rasilimali za mafuta na gesi asilia,” ameeleza Waziri Makamba.

Mabalozi waliofanya mazungumzo na Mh. Makamba ni pamoja na Balozi Abdulaziz Hamad Alasim (Saudi Arabia), Balozi Hussain Ahmad Al-Homaid (Qatar), Balozi Khalifa Abdulrahman M.A Almarzooqi (UAE), na Balozi Ahmed Djellal (Algeria).

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazungumzo hayo ni pamoja na Kamishna wa Petroli na Gesi Michael Mjinja, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Edward Sokoine na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) Dkt. James Mataragio.