Watumishi wa Umma Watakiwa Kuzingatia Mwongozo wa Mavazi
Na. James K. Mwanamyoto-Bariadi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Watumishi wa Umma nchini kuzingatia Mwongozo wa Mavazi kwa Watumishi wa Umma kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na.6 wa Mwaka 2020 wanapokuwa mahala pa kazi wakitekeleza majukumu yao.
Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo leo mkoani Simiyu alipokuwa akizungumza na Watumishi wa Umma wa Mkoa huo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani humo.
Mhe. Mchengerwa amesema, kuna baadhi ya Watumishi wa Umma katika taasisi mbalimbali za umma hawazingatii Mwongozo huo, na badala yake wanavaa mavazi yasiyostahili sehemu za kazi.
“Nawataka Watumishi wote wa Umma nchini kuzingatia Mwongozo wa Mavazi kwa Watumishi wa Umma kwa mujibu wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na.6 wa Mwaka 2020 wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao kwani kuna baadhi ya Watumishi hawauzingatii Mwongozo huu na kuvaa wanavyojisikia wao, jambo hili sitaki kuliona,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa ameainisha kuwa, mwongozo huo unafafanua aina ya mavazi yanayoruhusiwa na yasiyoruhusiwa kuvaliwa na Mtumishi wa Umma kulingana na eneo alilopo wakati akitekeleza majukumu yake.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewasisitiza watumishi kuacha matumizi ya simu wanapowahudumia wateja kwani kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa wananchi wanaofuata huduma na kuijengea taswira mbaya Serikali kwa wananchi wake.
“Kuna baadhi ya watumishi wamekuwa wakitumia simu na hata wakiona wateja bado wanaendelea kufanya hivyo badala ya kuwahudumia, ninawataka muache tabia hiyo mara moja, tufanye kazi kwa weledi, tujitoe kwa ajili ya wananchi, tuwasilikilize wananchi wanapofuata huduma, tuwajali maana nchi hii ni yao na tupo kazini kwa ajili yao,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa yuko Mkoani Simiyu kwenye ziara ya kikazi ya siku mbili kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF akitokea Mkoani Mwanza na Mara.