Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Watanzania 7,713 wanafanya kazi kwenye Mradi wa Bwawa la Kufulia Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) unaotekelezwa wilayani Rufiji, Mkoa wa Pwani.
 

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameyasema hayo leo jijini Mwanza alipokuwa akieleza kazi zinazofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
 

“Wafanyakazi 7,713 ambao ni sawa na asilimia 89 ya wafanyakazi wote 8,635 waliopo katika mradi huu ni Watanzania,” ameeleza Msigwa.
 

Sambamba na hilo, amefahamisha kuwa wakandarasi wanaotekeleza mradi huu wameshalipwa shilingi trilioni 2.832 ambayo ni sawa na asilimia 35.62 ya fedha zote shilingi trilioni sita na bilioni 558 zitakazotumika kugharimia ujenzi huu.
 

“Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango yeye wiki hii amefanya ziara katika mradi wa ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere katika mto Rufiji na kujionea kazi kubwa inayofanywa katika mradi huu,” amedokeza Msigwa.
 

Pamoja na hayo, Msemaji huyo amehabarisha kwamba mradi huu umebuniwa na kusanifiwa na Watanzania, na kwamba unasimamiwa na wahandisi wa Tanzania kupitia kitengo kilicho chini ya TANROADS kiitwacho TECU na unatekelezwa kwa fedha za Watanzania.
 

“Malighafi zinazotumika hususan tani 850,000 za saruji, tani 70,000 za nondo, tani 250,000 za pozzolana na malighafi nyingine zinatoka hapa hapa nchini kwetu,” amebainisha Msigwa.