Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetangaza kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaohusika na vitendo vya matumizi mabaya ya noti kwa njia yoyote ile ikiwemo kuwatuza watu kwa kuwarushia na kukanyagwa.
 
BOT imetoa tangazo hilo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa, kumekuwa na  vitendo vingi vya matumizi mabaya ya noti katika shughuli mbalimbali za kijamii hasa sherehe za harusi.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania na kusainiwa na Gavana wa benki hiyo Profesa Florens Luoga, baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kutuza kwa kurusha noti zinazoanguka sakafuni na muda mwingine kukanyagwa, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
 
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, baadhi ya watu wamekuwa wakiziviringisha noti katika maumbo mbalimbali na kutumia kama mapambo, kuweka kwenye mwili wa mtu ulio loa jasho huku wakijua kufanya hivyo ni kuvunja sheria.
 
BOT imewataka Watanzania wote kufuata maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa kuhusu namna sahihi ya kutunza noti zinazokuwa mikononi mwao na kuacha kuzitumia kinyume na maadili pamoja na matakwa ya kisheria.