Na WAMJW-MOROGORO
Serikali kupitia Wizara ya Afya itawachukulia hatua wote watakaobainika walihusika katika kuvujisha mtihani wa kitaaluma wa mwaka wa pili wa matabibu pindi tu ripoti ya uchunguzi itakapokamilika na kuwasilishwa.

Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati akizindua kituo cha Elimu masafa kilichopo Mkoani Morogoro.

“Serikali imeunda kamati ya uchunguzi iliyoshirikisha vyombo vyote, wakiwemo polisi na vyombo vyote vingine vinavyohusika na kuchunguza tuhuma kama hizi, ripoti ipo hatua za mwisho kukamilika, itasomwa wazi… maana wahalifu hao walichokitafuta watakipata…” Amesema Dkt. Gwajima.

Ameendelea kusema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya itachukua hatua hizo kwa kufuata Sheria, Kanuni na miongozo bila kuonea yoyote ili iwe fundisho kwa wengine wanaofanya vitendo hivi ambavyo ni kinyume na taratibu na Sheria  za nchi.

Mbali na hayo Dkt. Gwajima amesema kuwa, lengo la kufungua kituo hicho kwa njia ya mtandao ni kupunguza gharama za mafunzo na kuwafikia walengwa wengi zaidi katika kuendeleza ujuzi wao wa fani ya afya.

Hata hivyo ameyaelekeza Mabaraza kwa kushirikiana na Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuyatambua mafunzo haya na kuhamasisha wataalamu wao kutumia mfumo huo wa mafunzo kwa njia ya kimtandao ili kujiendeleza na kukuza ujuzi wao.

“Ninayaelekeza Mabaraza kwa kushirikiana na Waganga Wafawidhi wa vituo vya kutolea huduma za afya kuyatambua mafunzo haya na  kuhamasisha wataalamu wao kutumia mfumo huo wa mafunzo kwa njia ya kimtandao ili kujiendeleza na kukuza ujuzi wao.”Amesema Dkt. Gwajima.

Aidha, Dkt. Gwajima amesema kuwa, mafunzo kwa njia hii ya elimu masafa yatapunguza gharama na kusaidia kukabiliana na upungufu wa watumishi wa afya uliopo kwa kuwawezesha kujiendeleza kitaaluma wakiwa kwenye vituo vyao vya kazi.

Kwa upande mwingine amewaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kusaidia  kuboresha miundombinu ya kituo hiki ikiwemo maabara ya kisasa, hosteli kwa wanafunzi, madarasa, kumbi za mikutano na nyumba za wafanyakazi.

“Niwaombe wadau mbalimbali wa maendeleo kusaidia  kuboresha miundombinu ya kituo hiki ikiwemo maabara ya kisasa, hosteli kwa wanafunzi, madarasa, kumbi za mikutano na nyumba za wafanyakazi.”Amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo na Rasilimali watu Wizara ya Afya Dkt. Saitore Laizer amesema kuwa, Ujenzi wa kituo hiki umezingatia lengo na kitatumika kikamilifu ili tuweze kufikia malengo yaliyokusudiwa ambapo watumishi watapata fursa ya kujiendeleza wawapo maeneo yao ya kazi na kuongeza ufanisi kazini.

Aliendelea kusema kuwa, Mfumo huu umerahisisha utoaji wa mafunzo kwa watumishi wengi waliopo maeneo mbaimbali ya kutolea huduma, huku akiweka wazi kuwa, kutokana na changamoto ya UVIKO-19 mfumo huu umekuwa ukitumika kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa mafunzo ya ngazi ya kati nchini.