Waandamanaji wanaounga mkono jeshi nchini Sudan wamefunga kwa muda barabara kuu na madaraja katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum Jumapili, huku kukiwa na mvutano unaoongezeka kati ya majenerali na vuguvugu la kuunga mkono demokrasia lililochochea uasi huo dhidi ya rais wa zamani Omar al-Bashir.

Baadaye mchana, vikosi vya usalama viliwatawanya waandamanaji kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi na kufungua barabara zilizofungwa. 

Video kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha waandamanaji wakikimbia juu ya daraja na kwenye Mtaa wa Nile. 

Haya yanajiri siku moja baada ya Mjumbe Maalum wa Marekani kwa Pembe wa Afrika Jeffrey Feltman kukutana na viongozi wa kijeshi na kiraia mjini Khartoum kutafuta mwafaka katika mzozo huo.