Vijana Waaswa Kuenzi Waasisi Wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Na Sheikh Abeid Amani Karume
Na: Mwandishi Wetu – CHATO
Vijana nchini waaswa kuenzi na kuishi fikra za waasisi wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume ili waweze kuwa wazalendo sambamba na kudumisha tunu za Taifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameeleza hayo wakati wa ufunguzi wa Mdahalo wa Vijana Kitaifa uliofanyika katika Shule Sekondari Chato mkoani Geita tarehe 10 Oktoba, 2021.
Waziri Mhagama alieleza kuwa tunazo sababu za msingi za kuwakumbuka waasisi wa taifa hili ambao ni Baba wa Taifa na mwasisi wa mapinduzi ya Zanzibar hasa kwa mchango wake mkubwa usio sahaulika kwa Taifa letu.
“Mchango huu wa waasisi wetu ni vyema urithishwe kwa vizazi vilivyopo hususan vijana na vizazi vijavyo ili waweze kuwa wazalendo kwa taifa lao na wakaziishi falsafa za viongozi hao,” alieleza Waziri Mhagama.
Aliongeza kuwa vijana wanapaswa kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya Baba wa Taifa enzi za uhai wake na Sheikh Abeid Aman Karume ili waendelee kujivunia juu ya misingi ya amani na umoja iliyopo nchini.
Aidha alifafanua kuwa, Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kujenga umoja wa Kitaifa na kudumisha amani ya muda mrefu tuliyo nayo leo kama Taifa.
“Baba wa Taifa, aliasisi Mwenge wa Uhuru mwaka 1961 mara tu nchi yetu ilipopata Uhuru lengo lilikuwa ni kuutumia Mwenge wa Uhuru kama chombo cha kuhamasisha ujenzi wa Taifa lenye watu wenye amani, lenye watu wenye upendo, lenye watu wenye matumaini na lenye watu wenye heshima,” alisema
Pamoja na hayo alisisitiza vijana na wananchi kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuendeleza maono ya waasisi wa taifa na kuleta mageuzi ya kiuchumi yenye manufaa kwa taifa.
Waziri Mhagama alitumia fursa hiyo pia kuwahimiza wananchi na wakazi wa Chato kushiriki kwenye Maonesho ya Wiki ya Vijana ambayo yanafanyika katika Viwanja vya Mazaina sambamba na kushiriki kwenye kilele cha Mbio maalum za Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika Uwanja wa Magufuli Chato Mkoani Geita tarehe 14 Oktoba, 2021.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Rosemary Senyamule alisema kuwa ni vyema vijana wakatumia fursa ya mdahao huo ili waweze kutambua vyema historia ya Waasisi wa Taifa na kutambua maudhui ya Mwenge wa uhuru ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa kuwaunganisha watanzania na kuwahamasisha kufanya kazi kwa bidii ili wajiletee maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Mkoa, Richard Jaba akitoa salamu wakati wa mdahalo huo alisema ni heshima kubwa kwa vijana kupata fursa za kujumuika pamoja na kueleza masuala yao huku akipongeza uamuzi ya kuleta shughuli hizo katika mkoa wa Geita na kuwaasa vijana kuendeleza umoja, mshikamano na upendo ili kuendelea chukangia katika kuleta maendeleo nchini.
“Kalenda ya chama inatambua uwepo wa wiki la vijana, hivyo tunaunga mkono kwa vitendo uwepo wa mdahalo huu na tutaendelea kutoa ushirikiano kwenu pia tunashukuru kuleta shughuli hizi Geita.,”alisema Jaba ,