Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
SERIKALI ya Ujerumani imeipatia Tanzania msaada mwingine wa Euro milioni 45 sawa na takribani shilingi za Tanzania bilioni 119.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mitatu katika sekta za maji, afya na kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.

Msaada huo umekuja siku mbili tangu nchi hiyo iingie makubaliano mengine ya kutoa msaada wa kiasi cha Euro  milioni 71 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 190.5, kwa ajili ya kutekeleza miradi kadhaa ikiwemo maji, uendelezaji wa maliasili na utalii, afya ya mama na mtoto pamoja na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.

Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo mipya mitatu kwa niaba ya Serikali, na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mheshimiwa Regine Hess kwa niaba ya Ujerumani, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, alisema kuwa fedha hizo zitaisaidia nchi kukabiliana na athari za Uviko 19, kuboresha uhifadhi wa mazingira na huduma za jamii.

Alisema kuwa Mkataba wa kwanza uliosainiwa unahusisha mradi wa kuboresha upatikanaji wa maji na udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi na mradi wa kuboresha huduma za afya uliiotengewa kiasi cha Euro milioni 16.5 sawa shilingi bilioni 43.73.

“Katika fedha hizo kiasi cha Euro milioni 6 kitatumika kuboresha huduma ya maji kwenye Miji ya Mbeya, Songwe na Tunduma ambapo zaidi ya watu 500,000 wanatarajiwa kunufaika na huduma hiyo pamoja na kutoa ajira ya watu 2,000 katika sekta ya maji kwenye maeneo hayo”. Alisema Bw. Tutuba

Alifafanua kuwa mradi wa uboreshaji wa huduma ya afya umetengewa Euro milioni 10.5 na una lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika mikoa ya Tanga na Mbeya.

Bw. Tutuba alisema kuwa mradi mwingine unaofadhiliwa na Ujerumani una thamani ya Euro milioni 8.5 sawa na shilingi bilioni 22.53 zitakazotumika kwa ajili ya kufunga mitambo maalumu ya kidigitali itakayosaidia kudhibiti magari ya watalii yanayoingia kwenye Hifadhi za Taifa yasiharibu mazingira katika Hifadhi nne za Serengeti, Burigi-Chato, Katavi na Mikumi.

 “Mkataba wa tatu tuliosaini unahusisha msaada wa Euro milioni 20 sawa na shilingi za Tanzania bilioni 53 zilizotolewa kama fedha za dharura kwa ajili ya kukabiliana na upungufu wa fedha uliotokana na athari za ugonjwa wa UVIKO 19, katika sekta ya maliasili na utalii”. Aliongeza Bw. Tutuba.

Alieleza kuwa kusudi la mradi huo ni kufidia mapato yaliyopotea kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Misitu Tanzania (TAWA), katika maeneo tengefu katika Pori la Akiba la Selous na Hifadhi za Taifa za Serengeti na Nyerere.

Bw. Tutuba aliishukuru Ujerumani kwa kuwa rafiki mkubwa wa Tanzania ambapo mpaka sasa Serikali imenufaika na miradi mingi ya maendeleo iliyofadhiliwa na nchi hiyo katika Sekta za maji, afya, nishati, matumizi endelevu ya maliasili na uhifadhi wa mazingira, usimamizi bora wa fedha za umma na fedha za kuandaa miradi.

Kwa upande wake Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Mhe. Regine Hess, alisema nchi yake inajivunia uhusiano wa kindugu uliopo kati ya nchi yake na Tanzania ulifikisha miaka 60 sasa na kwamba nchi hiyo itaendelea kutoa misaada zaidi kwa nchi.

Alielezea umuhimu wa hifadhi ya mazingira katika maeneo ya hifadhi za taifa pamoja na kuboresha huduma za kijamii katika nyanja za maji na afya.

Naye Kiongozi wa Ujumbe wa Ujerumani uliofanikisha upatikanaji wa Msaada huo Bw. Marcus Von Essen, alisema Ujerumani imeamua kufufua ushiriki wake katika kujenga maendeleo ya Tanzania ili kuunga mkono uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita.

Kwa upande wake Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, aliishukuru Ujerumani kwa kusaidia sekta ya Hifadhi za Taifa nchini baada ya kuathiriwa kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo katika miaka miwili iliyopita shughuli za utalii zilikwama.

Alisema katika kipindi hicho ufanisi wa masuala ya utalii ulishuka kwa asilimia 72 na pia mapato yanayotokana na utalii yalishuka kutoka wastani wa dola za Marekani bilioni 2.6 hadi kufikia dola bilioni 0.715.

“Tuliomba misaada kwa nchi nyingi wahisani ili tuweze kukabiliana na athari hizo lakini ni Serikali ya Shirikisho la Ujerumani pekee limetupatia msaada ambapo hivi karibuni imetupatia msaada wa Euro milioni 20 na leo tumepewa fedha za nyongeza kiasi cha Euro milioni 15” Aliongeza Dkt. Ndumbaro.

Hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo imehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Allan Kijazi, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban na Meneja wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KFW) anayesimamia Kanda ya Mashariki na Umoja wa Afrika (AU), Bw. Gerald Kuehnemund.

Mwisho