Serikali ya Uingereza imeondoa zuio la kusafiri kwa abiria kutoka Tanzania na nchi zingine 46 zilizokuwa zimepigwa marufuku mapema mwaka huu kama njia ya kupunguza maambukizi ya aina mpya ya virusi vya corona.


Taarifa iliyotolewa jana Oktoba 7 imedai Tanzania imeondolewa katika orodha nyekundu kuanzia Oktoba 11 saa 4 asubuhi. Serikali ya Tanzania haijatoa kauli yoyote hatahivyo Uingereza imesema mpango huo utarahisisha watu wengi kusafiri kwenda nchi za ulaya.

Utaratibu huo pia unatoa nafuu kwa wenyeji wanaorudi Uingereza kutoka nchi hizo kwa kuwa hawatahitajika kukaa karantini.

Nchi nyingine ni Uganda, Afrika ya Kusini, Sudan, Burundi, Zambia, Zimbabwe, Somalia, Seychelles, Rwanda, Namibia, Msumbiji, Malawi, Lesotho, Mexico, Ethiopia, Eritrea, Eswatini DR Congo, Angola, Brazil, Botswana na Argentina.

Sababu za uamuzi huo ni kutokana na maendeleo ya chanjo kote ulimwenguni ambapo umeiwezesha Uingereza kupunguza orodha hiyo na kubaki na mataifa 7 tu.