Timu ya soka ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ imenyakua ubingwa wa michuano ya nchi za ukanda wa kusini mwa Afrika (Cosafa) 2021.

Twiga walioshiriki michuano hiyo kama wageni waalikwa, wamekinyakua kikombe cha ubingwa Jumamosi, tarehe 9 Oktoba 2021 nchini Afrika Kusini. Ni baada ya kuwafunga Malawi bao 1-0, lililowekwa kambani na Enekia Kasonga dakika ya 64.

Katika michuano hiyo, Twiga Stars imecheza michezo mitano ukiwemo wa fainali na kushinda yote mitano.

Aidha, Amina Allya wa Twiga Stars, amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo huku Janeth Simba wa timu hiyohiyo akinyakua tuzo ya kipa bora.

Mara baada ya Twiga Stars kutwaa ubingwa huo, pongezi zimetolewa na watu mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii akiwemo Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Kupitia ukurasa wa Twitter, Rais Samia ameandika “Naipongeza timu yetu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya COSAFA Wanawake 2021. Ubingwa huu unatuletea heshima, unaitangaza nchi yetu na kutia chachu kwa vijana wetu kushiriki michezo. Naipongeza TFF na wote walioshiriki kuiandaa timu yetu.”