Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa  Mohamed Omary Mchengerwa (Mb) amesema Tume ya Utumishi wa Umma itaendelea kuzijengea uwezo Taasisi za Umma na wadau kuhusu uzingatiaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, ili ziweze kutafsiri na kutekeleza ipasavyo Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Mchengerwa amesema hayo jana wakati akiwasilisha taarifa kuhusu utendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma kwenye Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI), kilichofanyika Ofisi za Bunge, Jijini Dodoma.

“Ili kuhakikisha malengo ya kuimarisha Utawala Bora yanafikiwa, Tume hupokea na kutolea uamuzi rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma na kufanya ukaguzi wa Uzingatiaji  wa Masuala ya Rasilimali Watu kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu katika Utumishi wa Umma. Aidha, Tume itaendelea kuzijengea uwezo Taasisi za Umma na Wadau  ili waweze kutafsiri na kutekeleza ipasavyo Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma” amesema Mheshimiwa Mchengerwa.

Akizungumzia Mamlaka ya Tume, alisema ili kuiwezesha kutekeleza majukumu yake katika Utumishi wa Umma, miongoni mwa Mamlaka ya Tume ni kuwachukulia hatua kupitia Mamlaka zao za Nidhamu Watendaji Wakuu wanaoshindwa kuwachukulia hatua Watumishi walio chini yao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia utendaji kazi katika Utumishi wa umma.

Kwa upande wao Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa  Abdallah Jafari Chaurembo (Mb) walisema bado kuna tatizo kwa baadhi ya Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka Nidhamu katika utekelezaji wa maagizo ya Tume.

“Watumishi wa umma waliosimamishwa au waliofukuzwa kazi na Waajiri au mamlaka zao za Nidhamu na kukata Rufaa Tume, pale inapoamuliwa na Tume na kuagiza warejeshwe kazini na shauri lianze upya tafsiri imekuwa ngumu katika utekelezaji wa maagizo ya Tume namna ya kufuata Sheria na Taratibu zilizowekwa katika kushughulikia na kuhitimisha mashauri ya Nidhamu”  alisema.

Wajumbe wa Kamati hiyo muhimu ya Bunge walisisitiza umuhimu wa matumizi ya TEHAMA kutekelezwa ipasavyo majukumu ya msingi ya Tume ili kuiwezesha Tume kushughulikia rufaa na malalamiko mengi na kufanya ukaguzi wa Rasilimali Watu kwa ufanisi zaidi.