Tanzania Umoja Wa Ulaya Zakubaliana Kuimarisha Uhusiano
Na mwandishi wetu, DSM
Tanzania, Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wa Jumuiya hiyo zimekubaliana kuendeleza uhusiano baina yao ambao umekuwepo kwa miongo kadhaa ya urafiki, ushirikiano na kwa maslahi ya pande zote.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya kukamilika kwa majadiliano ya pamoja kati ya Tanzania , Umoja wa Ulaya na Nchi wanachama wa Umoja huo yaliyofanyika jijini Dar es salaam tarehe 29 Oktoba 2021.
Katika majadiliano hayo Tanzania na nchi wanachaama wa Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuendelea kufanya kazi kwa pamoja katika kukuza demokrasia, haki za msingi na utawala wa sheria na kuunga mkono sera zinazolenga kuleta maendeleo endelevu.
Pande hizo pia zimeelezea umuhimu wa nafasi ya wanawake na vijana katika maendeleo endelevu pamoja na kuwawezesha na kujadiliania juu ya taarifa ya Tanzania ya mwaka ya haki za binadamu itakayowasilishwa katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa hivi karibuni.
Aidha Umoja wa Ulaya na Tanzania umekubaliana juu ya umuhimu wa maendeleo ya sekta binafsi na uwekezaji kama chachu ya ukuzaji wa uchumi na kutoa ajira kwa watu wengi na wamekubaliana kufanya kazi kwa pamoja ili kufanya mazingira ya biashara nchini yaweze kuvutia zaidi wawekezaji na kukuza biashara za nje kwa pande zote mbili. Pande hizo pia zimeelezea utayari wao wa kujadili masuala yanayoihusu Tanzania katika Mkataba wa ubia wa kibiashara kati ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kuhusu kuimarisha uhusiano zaidi katika siku za usoni pande hizo zimekubaliana juu ya umuhimu wa mpango wa ujirani, maendeleo na nyenzo ya ushirikiano wa kimataifa kama nyenzo mpya za kupata ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya na kusisitizia umuhimu wa Serikali ya Tanzania kusimamia na kutekeleza kikaamilifu miradi yote iliyo chini ya mpango huo
Pande hizo pia zimekubaliana kubadilishana taarifa juu ya mipango yao ya kisiasa na kijeshi katika jimbo la Cabo Delgado na kujadili juu ya madhara ya kibinadamu na kujadili mipango ya maendeleo katika nchi za Maziwa Makuu na zile za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Pia wamejadiliana kuhusu janga la ugonjwa wa Covid 19 katika maeneo yao na Umoja wa Ulaya umepongeza mwelekeo mpya wa sera ya afya ya Serikali ya Tanzania hasa katika hatua inazochukua za kutoa taarifa na kuchanja raia wake. Kikao hicho pia kimeeleza kutambua mpango wa Serikali ya Tanzania kutengeneza dawa zake yenyewe ikiwa ni pamoja na chanjo yake.
Kuhusu suala la ulinzi katika ukana wa bahari pande hizo zimejadiliana aina mbalimbali za uhalifu wa majini ambazo zikiwemo uvuvi haramu na kuelezea utayari wao juu ya kuchukua hatua za pamoja katika kutatua tatizo hilo.
Wamekubaliana kukutana na kufanya majadiliano ya pamoja angalau mara moja kwa mwaka ili kujadili masuala yanayowakabili wote kwa pamoja.
Majadiliano hayo ya Pamoja yamefanyika chini ya uenyekiti wenza wa Mkurugenzi mwendeshaji wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia masuala ya Afrika Balozi Rita Laranjinha na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na kuhudhuriwa Mawaziri na Makatibu Wakuu kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Majadiliano hayo pia yamehudhuriwa na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Alfredo Fanti na mabalozi kutoka nchi za Ubelgiji, Jamhuri ya Czech, Denmark, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Poland, Hispania na Sweden.