Na Mwandishi Wetu, Dar
Tanzania na Kenya zimedhamiria kumalizia kuondoa vikwazo vya kiutawala vilivyosalia ifikapo Disemba 2021 baada ya kuondoa vikwazo 46 visivyokuwa vya kikodi.

Hayo yamesemwa wakati wa mazungumzo baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa Kenya Nchini Tanzania Mhe. Dany Kazungu jijini Dar es Salaam ambapo takwimu zinaonesha urari wa biashara kati ya Nchi hizo umeongezeka mara sita zaidi baada ya kuondolewa kwa vikwazo hivyo.

Kutokana na hatua hiyo, Tanzania imeonekana kunufaika zaidi kwa kuondolewa kwa vikwazo hivyo kwa kuuza zaidi bidhaa zake nchini Kenya.

“Hii ni ishara nzuri kwa Tanzania lakini pia ni fursa kwa Tanzania na Kenya kuondoa umaskini kwa watoto wetu na ndugu zetu kupata ajira kwa wingi katika sekta ya biashara,” Amesema Mhe. Kazungu

Pia Balozi Kazungu amemueleza Waziri Mulamula kuhusu azma ya Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta kufanya ziara rasmi hapa nchini na kisha kuhudhuria sherehe za Uhuru tarehe 9 Disemba 2021 ambapo alialikwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipotembelea Kenya mapema mwaka huu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Tanzania inaheshimu makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa awali wa kuondo vikwazo hivyo na dhamira ni kuwa ifikapo Disemba 2021 vikwazo vya kiutawala navyo viwe vimeondolewa ili kukuza zaidi mahusiano ya Kidiplomasia na Biashara baina ya Tanzania na Kenya.

“Tumekubaliana kuhakikisha ifikapo mwezi Disemba 2021 vikwazo vyote vya kitawala viwe vimetatuliwa……….azma yetu ni kuhakikisha kuwa kila kitu kinakuwa sawa kwa Ustawi wa Diplomasia na biashara baina ya Tanzania na Kenya,” amesema Balozi Mulamula.

Katika tukio jingine, Balozi Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Mwakilishi wa Taasisi ya Sister Cities ya Marekani Bi. Ronda Pierce katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam