Na Mwandishi wetu, Dar
Tanzania na China zimeahidi kuendelea kuimarisha misingi ya uhusiano wa diplomasia baina ya mataifa hayo iliyodumu kwa zaidi ya miaka 50 kwa lengo la kukuza na kuendeleza maendeleo endelevu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili.

Ahadi hiyo imetolewa na Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Chen Mingjian, wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amesema kuwa pamoja na mambo mengine, wamejadili masuala mbalimbali ikiwemo suala la kukuza na kuendeleza misingi ya uhusiano wa kidiplomasia iliyowekwa wakati wa kuanzisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya mataifa haya 1964.

“Uhusiano wa Tanzania na China ni wa muda mrefu na umekuwa imara katika nyakati zote hii ni kutokana na kila taifa kuheshimu misingi ya taifa jingine na kutokuingilia masuala ya ndani ya taifa jingine, naamini kwa kuzingatia misingi hii uhusiano huu utaendelea kukua na kuimarika zaidi,” Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa wakati wote Tanzania na China zimekuwa na maelewano mazuri ambayo yamechangia kuimarisha diplomasia kwa mataifa hayo.

Balozi wa China hapa nchini, Mhe. Chen Mingjian, ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao imekuwa ikimpatia tangu aliwasili na kuongeza kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuendeleza ushirikiano wa kufanya kazi kwa pamoja kwa manufaa ya mataifa mawili.

“Naamini kuwa mimi ni kiungo cha kuimarisha na kuendeleza uhusiano baina ya China na Tanzania…..tumekuwa tukishirikiana katia sekta mbalimbali ikiwemo afya, kilimo, biashara na uwekezaji, miradi ya mikopo nafuu na misaada, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Uchukuzi, Utalii na utamaduni naahidi kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” Amesema Balozi Mingjian