Mamlaka ya Taliban jana, Jumamosi imeionya Marekani isiwavuruge, ukiwa ni mkutano wa kwanza wa ana kwa ana kufanyika tangu Marekani iondokea katika ardhi ya Afghanistan, huku kuongezeka kwa mauwaji ya kimadhehebu yakizusha maswali juu ya kushika kwao madaraka.

Baada ya mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Taliban, Amir Khan Muttaqi aliliambia shirika la habari la Afghanistan kwamba waliwaambia wazi kabisa kujaribu kuivuruga serikali ya Afghanistan haina tija kwa yeyote na kwamba uhusiano mzuri kwa taifa hilo ndio litakuwa jambo jema kwa pande zote.

Waziri huyo ambae pia alinukuliwa na Shirika la Habari la Ufaransa AFP aliongeza kusema hakuna sababu ya kuidhoofisha serikali iliyopo nchini Afghanistan, kwa kuwa hilo litasababisha matatizo kwa umma wa watu.

Wakati Taliban ikitafuta kutambuliwa kimataifa, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema ujumbe wa Marekani utaushinikiza utawala wa Taliban kuhakikisha magaidi hawaweki kambi zao nchini Afghanistan.