Timu ya Taifa Stars imefufua ndoto za kutinga hatua ya mwisho ya mtoano ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika huko Qatar mwakani baada ya jana kuwachapa wwenyeji Benin bao 1-0 Mchezo uliopigwa uwanja wa Stade de l’Amitie nchini Benin.

Shujaa wa Taifa Stars ni winga hatari wa klabu ya Wydad Casablanca Saimon Msuva  ambaye dakika ya 6 aliachia  shuti kali lililotinga moja kwa moja nyavuni.

Matokeo hayo yaliwafanya Stars, kufikisha pointi saba, sawa na Benin lakini kukiwa na utofauti wa mabao yakufungwa na kushinda.

Mchezo wa pili uliopigwa jana uliwakutanisha Madagascar ambao walikuwa nyumbani dhidi ya Jamhuri ya Congo, na wenyeji hao kufanikiwa kuondoka na ushindi wa bao 1-0.

Kipigo hiko kiliwafanya Congo kusalia na pointi zaao 5, kwenye nafasi ya tatu, huku Madagascar akiendelea kuburuza mkia akiwa na alama tatu, ukiwa ndio mchezo wao wa kwanza kushinda.

Kundi hilo sasa limebakisha michezo miwili kwa kila timu, ambayo itapigwa tarehe 11 na 14, Novemba 2021, ambapo Stars itaanza kushika Dimbani nyumbani dhidi ya Jamhuri ya Congo, na baadae wataenda ugenini kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Madagascar.