Sweden Yamwaga Bilioni 196 Kusaidia Sekta Ya Elimu Nchini
Na. Peter Haule, WFM, Dar es Salaam
Tanzania imepokea msaada wa Krona za Sweden milioni 750 sawa na shilingi bilioni 196 kwa ajili ya kusaidia utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Elimu kwa Matokeo unaohusu elimu ya Msingi (EPforR II).
Mkataba wa Msaada huo umesainiwa jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Anders Sjoberg kwa niaba ya Serikali ya Sweden.
Bw. Tutuba alisema kuwa mkataba wa msaada wa shilingi bilioni 196 uliosainiwa utasaidia utekelezaji wa mpango huo wa kuboresha elimu ya msingi kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Mwezi Julai, 2021 hadi Juni mwaka 2026.
Katika kutekeleza Mpango wa Elimu kwa Matokeo wa EPforR uliohusisha pia kuendeleza elimu ya msingi Awamu ya Kwanza, ulioanza mwaka 2014 hadi 2020, Sweden kupitia Shirika lake la Maendeleo SIDA, ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 208.
“Nakumbuka tarehe 26 Agosti, 2021 tulisaini Mkataba mwingine wa Msaada wa Krona za Sweden milioni 450 sawa na shilingi bilioni 118 kwa ajili ya Mpango wa pili wa kunusuru Kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, tunaishukuru Serikali ya Sweden kwa ushirikiano huu” alisema Bw. Tutuba
Bw. Tutuba aliyataja baadhi ya mafanikio ya utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mpango huo kuwa ni ujenzi wa madarasa, 10,409, mabweni 646, nyumba za walimu 91, majengo ya utawala 37, maktaba 49, maabara 29, uzio 3 na visima vya maji katika shule za msingi 16.
Aliyataja mafanikio mengine kuwa ni ujenzi wa ofisi 155 za udhibiti wa ubora wa shule, ujenzi wa shule mpya 44, ukarabati wa shule kongwe 86, ununuzi wa magari 347 kwa ajili ya halmashauri zote za wilaya, ofisi za wilaya za udhibiti wa ubora wa shule, maafisa elimu wa mikoa, Baraza la Mitihani la Taifa na vyuo vya elimu.
Bw. Tutuba aliihakikishia Serikali ya Sweden kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, itaendeleza ushirikiano na Serikali ya Sweden kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania Mhe. Anders Sjoberg, alisema kuwa nchi yake inafadhili kwa mara nyingine uboreshaji wa elimu ya msingi ambapo mpango huo umelenga kuwanufaisha wanafunzi milioni 16.
Alibainisha kuwa mpango wa awali ulilenga zaidi kuwanufaisha Watoto wa kike lakini mpango huu mpya utawanufaisha wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum na kuwawezesha kuhitimu masomo yao kwa ajili ya manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Sjoberg alisema kuwa EPforR Awamu ya Kwanza imefanikisha kujenga mifumo imara ya elimu ya msingi kwa kuweka miundombinu mahsusi na maendeleo ya kimkakati itakayoisaidia nchi kuboresha elimu kwa miongo mingi ijayo.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkataba wa msaada huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo, alisema kuwa watahakikisha fedha hizo zinatumika ipasavyo na watasisimamia kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwenye miradi itakayokuwa ikitekelezwa kupitia ufadhili huo.
Aliahidi kuwa msada uliotolewa utawezesha malengo yaliyotarajiwa katika sekta ya elimu inayotaka kila mtoto anapata elimu bora yanafikiwa kama inavyoelekezwa kwenye mpango wa Maendeleo wa Taifa na mikataba mingine.
Mpango wa Elimu kwa matokeo EPforR unafadhili kwa pamoja na Benki ya Dunia, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden (SIDA), Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Korea (KOICA) na Shirika la Elimu Duniani (GPE) kwa kutumia mfumo wa mpango kwa matokeo kuleta mabadiliko yenye tija katika Sekta ya Elimu Msingi nchini Tanzania