Na Faustine Gimu:
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai leo anatarajia kufungua rasmi wiki ya Asasi za Kiraia(AZAKI)ambapo jumla ya Asasi zaidi ya 150 zitashiriki katika maonyesho ya wiki hiyo lengo likiwa ni kuonyesha mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Hayo yameelezwa jana Jijini Dodoma na Mkurugenzi mkazi wa Christian Blind Mission (CBM) Tanzania,Nesia Mahenge wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kuelekea wiki ya AZAKI ambayo itatanguliwa na matembezi ya amani yatakayoanza saa moja asubuhi kuanzia shule ya sekondari Dodoma hadi uwanja wa Jakaya Kikwete.
Aidha amesema ,pamoja na mambo mengine wiki hii inawakutanisha wadau mbalimbali wa Maendeleo nchini ikiwemo Wananchi,Serikali,AZAKI na sekta binafsi ambao wote kwa pamoja watajadili na kusherehekea mchango wa AZAKI katika kuleta maendeleo nchini ambapo kutakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo huduma ya msaada wa Sheria.
Sambamba na hilo amesema katika kuunga juhudi za Serikali mapambano dhidi ya UVIKO19 watakuwa na Banda Maalum la kutoa huduma ya chanjo ya Uviko kwa wananchi na kutaka kujitokeza.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa United Nations Association (UNA) Reynald Maeda ameeleza kuwa maendeleo yanayoletwa na AZAKI si maendeleo ya kifedha tu bali katika maeneo mengine ikiwemo maendeleo ya wanachi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo kuongeza ushirikishwaji wa watu wote kwenye jamii,kupinga ukatili wa kijinsia Kwa wanawake na Watoto pamoja na kuongeza nguvu katika ufuatiliaji wa rasilimali za umma.
Wiki ya AZAKI hukutanisha wadau wa maendeleo kujadili masuala ya masingi kuhusu ustawi wa sekta pamoja na maendeleo ya Taifa Kwa ujumla na utawashirikisha viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali wakiwemo mabalozi wa Canada Nchini Tanzania na Balozi wa Denmark Nchini Tanzania pamoja na Balozi wa Sizaland Nchini Tanzania na itaadhimishwa Oktoba 28 Mwaka huu.
Mwisho