Spika wa Bunge, Job Ndugai, amefanya mabadiliko madogo ya wajumbe wa kamati za kudumu za Bunge kwa kuzingatia matakwa ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni 2020.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Ofisi ya Bunge, mabadiliko hayo yanawagusa wabunge: Godwin Kunambi anayehamishwa kutoka Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwenda Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Humphrey Polepole anayehamishwa kutoka Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa kwenda Kamati ya Sheria Ndogo.

Kutokana na mabadiliko hayo, Polepole ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa, anapoteza nafasi aliyokuwa nayo ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa.

Mabadiliko yaliyofanywa na Spika Ndugai pia yamewagusa wabunge: Asia Halamga, aliyeteuliwa kuwa Mjumbe ya Kamati ya Masuala ya UKIMWI; Dk. Faustine Ndugulile aliyeteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo na Kamati ya Masuala ya UKIMWI.

Aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo; aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Sheria Ndogo; na Agnes Marwa ameteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati ya Masuala ya UKIMWI.