Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, imetenga shilingi Bilioni 7.4 kwa mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya kuboresha Makazi ya Wazee nchini.

Taarifa hiyo imetolewa jana  jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akiwasilisha taarifa ya Makazi ya wazee mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Mhe. Dkt. Gwajima amesema, lengo la Bajeti hiyo ni kuendeleza mpango wa Wizara katika kukabiliana na changamoto ya uchakavu wa Miundombinu kwenye makazi hayo na kuweka mazingira mazuri kwa Wazee wanaoishi katika Makazi hayo.

“Mojawapo ya vigezo kwa mujibu wa mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa makazi ya wazee ni kuwa na mazingira wezeshi kwa wazee wasiojiweza pamoja na vifaa vya kumudu kupata huduma ndani na nje ya makazi, hivyo Wizara imejipanga kuhakikisha makazi yote 14 yanayosimamiwa na Serikali yanakidhi vigezo hivyo, ikiwemo majengo, umeme, maji safi na mifumo ya maji taka”. Amesema Mhe. Gwajima.

Dkt Gwajima ameongeza kuwa jumla ya wazee 2,135 wamepata matunzo katika Makazi ya Wazee katika kipindi cha mwaka 2015 - 2020 na Serikali inasimamia na kuratibu utoaji wa huduma kwa wazee katika makazi 20 yanayoendeshwa na Taasisi binafsi pamoja na Mashirika ya Dini yenye jumla ya wazee 537.

Aidha, Mhe. Dkt. Gwajima amewahimiza wananchi au Taasisi zinazolenga kuanzisha makazi ya wazee kuzingatia taratibu wakati wa kuanzisha makazi hayo kwa kushirikisha mamlaka za maeneo husika ili kuweza kuhakikisha vigezo vyote vimezingatiwa.

Ameyataja mafanikio ya Wizara katika kuendesha makazi hayo kuwa baadhi ya makazi yameboreshwa miundombinu yake yakiwemo nyumba na miundombinu mingine ambapo Makazi yaliofanyiwa ukarabati huo ni Nunge (Dar es Salaam), Kolandoto (Shinyanga), Njoro (Kilimanjaro), Magugu (Manyara), Kiilima (Kagera), Fungafunga (Morogoro) na Sukamahela (Singida).

"Huduma za chakula na mahitaji ya msingi zimeboreshwa pamoja na kuanzisha miradi ya bustani na ufugaji ambayo hutekelezwa na kusimamiwa na wazee wenyewe" alisisitiza Waziri Dkt. Gwajima

Akifafanua Masuala mbalimbali kuhusu Makazi ya Wazee Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike amesema hadi sasa katika Makazi ya Wazee 14 yanayohudumiwa na Serikali kuna jumla ya watumishi 93 wa kada mbalimbali ambapo kati yao maafisa ustawi wa jamii ni 19.  

" Niseme tu tunaratibu pia uendeshaji wa Makazi ya Wazee binafsi na jumla ya makazi 20 yanayomilikiwa na taasisi binafsi pamoja na mashirika ya dini yameajiri jumla ya watumishi 88 wa kada mbalimbali ambao wanasimamia na kutoa huduma kwa wazee.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii, Mwanaisha Moyo amesema Wizara kupitia Idara hiyo imejipanga kuhakikisha inawahudumia wazee waliopo katika makazi ya wazee yanayosimamiwa na Serikali nchini ili kuhakikisha wanaishi vizuri na kupata mahitaji yote muhimu.