Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuwekeza zaidi ya dola za Kimarekani bilioni 5.5, sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni 12.6 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Dkt. Nchemba ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, wakati wa Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), iliyofanyika kwa njia ya mtandao, Jijini Dar es Salaam.

“Miongoni mwa fedha hizo ni pamoja na kiasi cha dola za marekani bilioni 1.167 zilizotolewa na Benki hiyo kwa ajili ya kutekeleza miradi mitano ya maendeleo ikiwemo ya sekta ya elimu, miundombinu, umeme na Tanzania ya Kidijitali kwa lengo la kuchochea uchumi jumuishi na kupambana na umasikini” Alisema Dkt. Nchemba

Dkt. Nchemba alisema kuwa kiasi hicho cha fedha kinahusisha utekelezaji wa miradi 26 ya maendeleo inayopata fedha kupitia dirisha la mikopo nafuu (IDA) la Benki ya Dunia yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5.502.

Alisema kuwa miradi 21 kati ya hiyo ni ya kitaifa yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 4.804 na miradi 5 ni ya Kikanda yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 0.698 na kwamba mpaka sasa kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.932 kimetolewa na Benki hiyo sawa na asilimia 35 ya fedha zote.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali kupambana na athari za kiuchumi na kijamii zilizosababishwa na ugonjwa wa UVIKO-19, Dkt. Mwigulu Nchemba alisema kuwa Serikali imeandaa mpango wa mwaka mmoja wa kukabiliana na athari za ugonjwa huo utakaogharimu shilingi trilioni 3.62

“Tayari Serikali imepokea dola za Kimarekani milioni 567.25 sawa na takribani shilingi za Tanzania trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ukiwa ni mkopo nafuu kwa ajili ya kunusuru maisha ya watu pamoja na uchumi wa nchi kutokana na athari hizo za UVIKO-19” alieleza Dkt. Nchemba.

Alisema kuwa fedha hizo zimeelekezwa kutatua changamoto za athari za UVIKO-19 kwenye sekta ya utalii, kunusuru kaya masikini, maji, elimu na Afya upande wa Tanzania Bara na Zanzibar na akatoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kuunga mkono jitihada hizo za Serikali ili kusisimua uchumi wa nchi.

Amesema kuwa hivi karibuni Serikali inatarajia kukamilisha mazungumzo na Benki ya Dunia kwa ajili ya kupata fedha za miradi miwili ikiwemo mradi wa kuboresha masuala ya ardhi na kuongeza msukumo wa kujifunza kupitia elimu ya msingi.

Kuhusu suala la wanafunzi wanaoacha masomo, Dkt. Nchemba alimwambia Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia Dkt. Hafez Ghanem kwamba changamoto ni kubwa ambapo takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi (wasichana na wavulana) 198,620 waliacha masomo katika shule za msingi wakati wanafunzi 113,484 wa shule za sekondari waliacha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo vifo, utoro, utovu wa nidhamu na ujauzito.

“Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kuanzishwa kwa mradi wa kuboresha elimu ya Sekondari (SEQUIP) na mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya msingi unaoombewa fedha kutoka Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo.

Akizungumza katika Mkutano huo, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayezisimamia nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, aliipongeza Tanzania kwa hatua mbalimbali inazozichukua katika kusimamia uchumi na maendeleo ya wananchi wake.

Aliahidi kuwa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Dunia itakutana hivi karibuni kujadili maombi mbalimbali ya fedha yaliyotolewa na Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi  ya maendeleo ili fedha hizo zipatikane kwa wakati.

Dkt. Ghanem alishauri masuala kadhaa yafanyiwe kazi na Serikali ikiwemo kuongeza jitihada ya kuyasaidia makundi maalumu yakiwemo ya vijana na wanawake ili waweze kujengewa uwezo wa kiuchumi pamoja na kukuza ajira.

Alisema pia kuwa suala la wasichana wanaopata ujauzito wakiwa shuleni wajengewe mazingira ya kuendelea na masomo baada ya kujifungua, suala ambalo Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alimweleza kuwa Serikali inalifanyia kazi na kuangalia utaratibu utakaofaa zaidi kushughulikia suala hilo.

Aidha, Makamu wa Rais huyo wa Benki ya Dunia alipongeza utaratibu mzuri ulioanzishwa na Serikali wa kuimarisha na kuishirikisha sekta binafsi katika kutekeleza miradi mikubwa na ya kimkakati ya maendeleo kupitia mpango wa ushirikiano wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.