Na Ahmed Sagaff – MAELEZO
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Serikali kupitia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) imeandaa mbinu kabambe utakaowasaidia wastaafu kupata malipo yao kwa wakati.
 

Akizungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari jijini Mwanza leo, Msigwa amezitaja mbinu hizo kuwa ni ‘Data Cleanup’ na ‘Lipa Jana’.
 

“Na sasa PSSSF inakwenda kwa kauli mbiu isemayo “Lipa Jana” yaani wanataka mtu ukistaafu leo mafao yako yawe tayari yameshaingia kwenye akaunti yako tangu jana,” ameeleza Msigwa.
 

Akiifafanua mbinu iitwayo ‘Data Cleanup’, Msigwa amefahamisha kwamba ubunifu huu utaiwezesha PSSSF kuweka sawa taarifa za wafanyakazi kabla ya tarehe ya mwisho ya kustaafu.
 

“Lengo mtu anapostaafu kusiwe na mambo hayajakaa sawa katika taarifa zake za utumishi,” amebainisha Msigwa.