Ibrahimu Hamidu

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Uwekezaji imewakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nchini Misri kupitia Jumuiya ya Muungano Kimataifa chini ya kundi la Afrika na Asia (Afro-Asian Union (AFASU). Ujumbe wa Jumuiya hiyo umefika nchini kwa ajili ya kuangalia fursa za uwekezaji hususani katika sekta ya; Utalii, Kilimo, Afya, Elimu na TEHAMA.

Akiongea wakati wa kikao na wawekezaji hao leo tarehe 7 Oktoba, 2021, ofisini kwake jiijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Geoffrey Mwambe amewahakikishia wawekezaji hao kuwa ofisi hiyo itaratibu shughuli za uwekezaji wanazo kusudia kuzifanya hapa nchini kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji hao.

Aidha, Mhe. Mwambe amebainisha kuwa wito wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kuwataka wawekezaji waje kuwekeza katika sekta yoyote waliyo na uwezo wa kuwekeza nchini. Ameongeza kuwa ujio wa wekezaji hao ni matokeo ya ziara aliyoifanya nchini Misri, mwezi Juni mwaka huu, ambapo aliwaalika kufanya ziara ya kibiashara nchini ili waweze kuona fursa za biashara na uwekezaji.

Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya hiyo, Dkt.Hossam Darwish amefafanua kuwa Jumuiya hiyo imekusudia kuanza uwekezaji hapa nchini kuanzia mwaka huu kwa kuwa tayari wameshakamilisha utafiti wao wa masuala ya biashara na Uwekezaji.Amebainisha kuwa wanahitaji kuanza na ujenzi wa chou Kikuu cha masuala ya TEHAMA.

Aidha, ameongeza kuwa Jumuiya hiyo itajikita katika uwekezaji wa masuala ya Utalii hususani katika ujenzi wa Hoteli zenye hadhi kubwa. Katika sekta ya Afya ameeleza kuwa watajikita katika ujenzi wa Viwanda vya kuzalisha Dawa na Vifaa tiba, Ujenzi wa Hospitali ya Macho na teknlolojia ya Huduma ya Hospitali inayotembea.

Dkt. Hossam amebainisha kuwa wanao mpango wa kuandaa maonesho makubwa maalum ya Biashara na uwekezaji hapa nchini, ili kuweza kuchochea uwekazaji wenye tija. Aidha, ameeleza kuwa Jumuiya hiyo inayo teknolojia ya kisasa ya usindikaji taka za ambayo wanaweza kuiwekeza hapa nchini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu- Uwekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na Ubalozi wa Misri.

Jumuiya ya AFASU ilianzishwa mwaka 1957, ambapo kwa sasa Jumuiya hiyo inao wananchama katika nchi 52 za Afrika na Asia. Miongoni mwa malengo ya Jumuiya hiyo ni kuunganisha nchi za Afrika na Asia katika Sekta ta Elimu, Uwekezaji na Biashara, kutafuta mitaji na kutekeleza miradi kati ya Sekta Binasi na  serikali.