Happy Lazaro,Arusha
Arusha .Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh Samia Suluhu  Hassan leo anatarajiwa kupokea ndege mbili aina ya Airbus ambapo ndege hizo moja itapewa jina la Zanzibar na nyingine Tanzanite.
 

Akizungumza  na waandishi wa habari mkoani Arusha jana  Waziri wa ujenzi na  uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa ,ndege hizo zitapokelewa Zanzibar ambapo kila ndege itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 132, huku abiria 12 wakiwa ni daraja  la biashara na 120 wakiwa ni daraja la uchumi.
 

“Ndege hizi zina mfumo wa kisasa na zimeongezewa uzito hasa wakati wa kuruka kutoka Tani 67 hadi kufikia tani 69.9 lakini pia ina viti vya kisasa ambavyo vitawafanya abiria kustarehe zaidi ambapo baada ya kuzipokea hizo mbili kesho Tanzania tutakuwa na jumla ya ndege 11,” amesema Profesa Mbarawa.
 

Amefafanua kuwa, pia ndege hizo zitakuwa na burudani za watoto, muziki, sinema na internet na hivyo kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hiyo kwa maendeleo ya nchi yetu.
 

Profesa Mbarawa amesema kuwa, ndege hizo zikiwa angani zina mifumo ya kisasa  ambayo inamwezesha rubani kufanya kazi kwa ufanisi wa hali ya juu.