SERIKALI inatarajia kutangaza ajira za wahandisi 260 ili kujaza nafasi zilizo wazi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Aidha, inaendelea na mchakato wa kuandaa ajira za watendaji wa kata, mitaa na vijiji baada ya kukamilisha tathmini ya mahitaji halisi yaliyopo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ziara aliyoifanya hivi karibuni Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu.

Alisema katika ziara hiyo alibaini kero mbalimbali za kiutumishi ikiwamo upungufu wa watumishi hususan Maofisa Ugani, Watendaji wa kijiji, Wahandisi, Mafundi Sanifu, Madereva, Makatibu Mahsusi, Wasaidizi wa Kumbukumbu na kada zingine.

“Nimshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kutoa kibali cha ajira kwa wahandisi 260 ambapo ajira hizi kwa mujibu wa taratibu za utumishi tunaendelea na taratibu ili watumishi hawa waajiriwe na kupelekwa kwenye wilaya zetu zote nchini.”

“Katika maeneo mengi niliyopata fursa ya kupita na kuzungumza na watumishi nimepokea kero ya upungufu mkubwa wa watumishi kwenye mikoa na wilaya, kuna maeneo yameonekana kuwa na watumishi wengi, kuna haja sisi wizara kujipanga vizuri ili kuangalia maeneo yale ambayo watumishi ni wengi kwenye baadhi ya kata, wapelekwe maeneo yenye uhaba mkubwa,” alisema.

Alisema serikali imetoa fedha nyingi za miradi mbalimbali na uwapo wa watumishi wa kada ya uhandisi watasaidia kusimamia fedha hizo.

Kadhalika, alisema serikali itaendelea kutenga bajeti kwa nafasi za msingi zenye upungufu kwa ajili ya kujaza nafasi husika kwa awamu kulingana na uwezo wa kibajeti.

Aliwaagiza waajiri kuendelea kushughulikia watumishi wenye vigezo na sifa za kupandishwa cheo kwa kuwatengea bajeti katika mwaka wa fedha ujao.

“Pia kushughulikia malipo stahiki ya watumishi ikiwamo malimbikizo ya mishahara, waajiri wanatakiwa kuingiza madai ya malimbikizo ya mishahara katika Mfumo wa HCMIS kama ilivyoelekezwa katika Waraka wa Utumishi wa Umma namba moja wa mwaka 2021,” alisema.

Alimwagiza Katibu Mkuu Utumishi kuandaa pia waraka kwa Maofisa Utumishi ili kufanya vikao vya kusikiliza kero za watumishi na kuzitatua kila baada ya robo mwaka.

“Naagiza kuwasilishwa kwa orodha ya watumishi wenye sifa za kukaimu ili ofisi hiyo ikamilishe mchakato wa kujaza nafasi wazi za idara na vitengo na hapa nasisitiza lifanyike bila upendeleo na unyanyasaji kwa watumishi,” alisema.

Katika ziara hiyo, Waziri Mchengerwa alibaini viongozi kutoa siri kuhusu matokeo ya upekuzi kwa maofisa waliopendekezwa kuteuliwa kwenye nafasi za uongozi.

Alisisitiza kuimarishwa kwa mifumo ya utunzaji wa siri za serikali ikiwa ni pamoja na kutekeleza viapo vya utunzaji siri ili kuzuia uwezekano wa uvujaji wa siri.

Credit:IPP