Serikali Imepanga Kufanya Maboresho Makubwa Bohari Ya Dawa (MSD)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imepanga kufanya maboresho ya kiutendaji katika Bohari ya Dawa (MSD) ili kuhakikisha wananchi wanapokwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wanapata dawa.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la maboresho hayo ni kuhakikisha dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikisha dawa na vifaa tiba vinapatikana nchini kote inatimia.
Ameyasema hayo jana (Jumanne, Oktoba 5, 2021) wakati akizungumza na watumishi, madiwani na wananchi wa halmashairi ya Mtama mkoani Lindi akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mtama, Dkt. Dismas Masulubu ambaye alisema walipeleka shilingi milioni 300 Bohari ya Dawa mwaka wa fedha uliopita kwa ajili ya ununuzi wa dawa lakini hadi sasa hawajapelekewa.
“…MSD inatakiwa ifanyiwe maboresho kwa sababu wanalipwa fedha kwa ajili ya dawa na vifaa lakini dawa hazipatikani kwa wakati. Dhamira ya Mheshimiwa Rais Samia ni kuhakikisha dawa zinapatikana katika maeneo yote ya kutolea huduma.”
Waziri Mkuu ameiagiza MSD ihakikishe inapeleka dawa katika maeneo yote kwa wakati pamoja na kulipa madeni yote dawa inayodaiwa na baadhi ya hospitali, vituo vya afya na zahati ili wananchi wapate huduma kama ilivyokusudiwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameweka mikakati madhubuti inayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote nchini yakiwemo ya Halmashauri ya Mtama.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza kampeni ya Mheshimiwa Rais Samia ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana karibu na makazi yao lengo likiwa ni kuwawezesha wanawake na vijana kupata muda wa kushiriki katika shughuli za kijamii.
Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti yenye lengo la kumaliza tatizo la maji nchini, hivyo wananchi wawe na subira na waendelee kuiunga mkono Serikali yao kwa kuwa imedhamiria kuwahudumia.