Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema, Serikali anayoingoza inakamilisha mchakato wa kuifanya Chato kuwa Mkoa.

Amesema hayo jana Alhamisi, tarehe 14 Oktoba 2021, katika Uwanja wa Magufuli, Chato mkoani Geita katika kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru na Kumbukumbu ya kifo cha miaka 22 ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Pamoja na kuwaombea, Marais wastaafu, Benjamin Willium Mkapa na John Pombe Magufuli, Rais Samia alisema, katika kumuenzi Hayati Magufuli aliyefariki dunia 17 Machi 2021, akiwa madarakani, walimua shughuli hizo kitaifa, zifanyikie wilaya ya Chato, sehemu aliyozaliwa Hayati Magufuli.

“Tumesukumwa na uamuzi wa kuja Chato ili kumuenzi mpendwa wetu Hayati Magufuli ambaye ni mzaliwa wa Chato, aliyepapenda sana nasi tunaendeleza upendo wake. Ili kumuenzi tumeamua kuja kufanya sherehe hizi ambazo kwa kawaida hufanyika makao makuu ya mkoa,” amesema Rais Samia huku akishangiliwa.

Ametumia fursa hiyo kuwaeleza kuwa “yapo mambo ambayo Hayati Magufuli aliwaahidi wana Chato wakati wa kampeni. Mambo hayo ni upanuzi wa Bandari ya Nyamilembe, kumamilisha Uwanja wa Ndege wa Chato, Hospitali ya Kanda ya Chato, Chuo cha Veta na mimi niwaahidi yote yatatekelezwa.”

Huku shangwe zikitawala uwanjani hapo, Rais Samia akasema, lipo jambo ambalo wananchi wa Chato wangependa kulisikia kutoka kwake. Kauli hiyo ilizidisha shangwe zaidi na yeye akasema “Serikali inakamilisha vigezo vinavyoruhusu Chato kuwa Mkoa. Kuna vigezo kadhaa ambavyo bado tunaendelea kuviangalia na vigezo hivi vikikidhi tunakwenda kulimaliza jambo hili.”