Rais Samia Suluhu Hassan ameishukuru kampuni ya Royal Dutch Shell yenye makao yake makuu nchini Uholanzi kwa nia yake ya kutaka kuwekeza kwenye mradi wa gesi asili iliyosindikwa (LNG) ambao utachochea kukuza uchumi wa Tanzania.
 
Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shukrani hizo wakati akizungumza kwa njia ya mtandao na afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo Ben Van Beurden.
 
Wakati wa mazunguzmo hayo ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameyafanya akiwa Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, Van Beurden ameeleza kuridhishwa na jinsi Serikali ilivyoboresha mazungumzo ya uwekezaji kwenye mradi huo wa gesi asili iliyosindikwa hapa nchini.
 
Wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo ni Waziri wa Nishati January Makamba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Katibu Mkuu wa wizara ya Nishati Mhandisi Leonard Masanja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio.