Rais Samia Suluhu Hassan amezindua vituo jumuishi vya utoaji wa haki ambavyo vimejengwa kwa thamani ya Sh51 bilioni katika mikoa mitano nchini.
Uzinduzi huo umefanyika leo Oktoba 6 2021 katika jengo la Dodoma likiwakilisha majengo mengine yaliyojengwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Morogoro na Arusha.
Akizungumza Mtendaji Mkuu wa Mahakama Profesa Elisante Gabriel amesema fedha kwa ajili ya ujenzi huo zimetolewa na Benki ya Dunia (WB).
Amesema kituo hicho kinajumuisha wadau mbalimbali wakiwemo mawakili, mwendesha mashitaka mkuu wa Serikali (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), jeshi la Magereza, Ustawi wa Jamii.
Amesema pia jengo hilo litakuwa na eneo la kunyonyeshea watoto pindi mama zao wanapokuwa wanafika kwa ajili ya kupata huduma kwenye jengo hilo.Aidha, amesema kuna upungufu wa mahakama 2996 nchini.
“Mahakama za mwanzo zipo 960 na zinatakiwa kuwa kila kata. Kwa mujibu wa Tamisemi (Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) zinaonyesha kuna kata 3956 kata za nchini kwa hiyo upungufu ni mahakama 2,996,” amesema.
Amesema kuna wilaya 139 lakini mahakama za wilaya zipo 119 na hivyo upungufu ni mahakama 20.
Kwa upande wa watumishi wa mahakama amesema wapo watumishi 5,835 na kwamba watumishi 10,350 wanahitajika ili kuziba pengo hilo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palagamba Kabudi amesema watapeleka maombi maalum kwa Rais Samia ya watumishi wa mahakama na maeneo mengine ya wizara yake.