Rais Samia Aipongeza Wizara Ya Utamaduni, Sanaa Na Michezo Kwa Ubinifu
Na. John Mapepele, WSUM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ubunifu wa kuandaa mikakati mbalimbali ya kuendeleza sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo ikiwa ni pamoja na kuandaa Tamasha kubwa la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linaoanza kesho oktoba 28 hadi 30 mjini Bagamoyo.
Rais Samia ameyasema hayo Oktoba 27, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam kwenye hafla maalum aliyoiandaa kwa ajili ya kuipongeza Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake (Twiga Stars) kwa kutwa Kombe la COSAFA hivi karibuni.
“Ili kufanikisha ushindi naomba nitambue TFF, Wizara na Wadau wengine hongereni kwa umoja wenu, najisikia fahari Twiga Stars kushinda ugenini na kuleta kombe nyumbani” amefafanua Mhe. Rais
Tamasha la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lenye kauli mbiu isemayo “Sanaa ni Ajira” lina lengo la kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni wa mtanzania pia kukutanisha watu wa tamaduni tofauti kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kuonyesha utajiri wao wa sanaa na utamaduni.
Rais Samia pia amepongeza ubunifu na uratibu uliofanywa wa kuandaa Tamasha la Michezo kwa Wanawake la Tanzanite lililofanyika hivi karibuni jijini Dares Salaam.
Amesema wakati akikabidhiwa uchifu hivi karibuni na Umoja wa Machifu nchini mkoani Mwanza aliiagiza Wizara kuwa na Tamasha la Uchifu ambalo litakuwa likizunguka kila mkoa na kuwataka machifu washirikishwe kikamilifu ili kukuza utamaduni ndani ya nchi yetu.
Ameongeza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatika kwenye sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo katika kipindi hiki ni kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ambapo amesema Serikali ilitenga 1.5 bilioni na kiasi kingine kimetoka kwenye michezo ya kubashiri.
Ameipongeza Wizara kwa kuratibu Tamasha kubwa la Bara la Afrika la warembo, mitindo na watanashati ambalo limetoa washindi sita kwenda kwenye mashindano hayo kidunia nchini Brazil Aprili 2022 na kuitaka Wizara ianze maandalizi kwa ajili ya washiriki hao mapema ili waende wakiwa wanajiamini.
Mhe. Rais ametumia tukio hilo kuzipongeza Timu za Kriketi za wanaume na wanawake zilizoshika nafasi ya tatu katika shindano la Bara la Afrika na kuitaka Wizara kuupa kipaumbele mchezo huo ili uweze kufika kwenye ngazi ya kimataifa.
Pia ameipongeza Timu ya Soka ya Wanawake ya Taifa chini ya umri wa miaka 20 kwa kuendelea kufanya vizuri kwenye mashindano ya kuelekea kombe la dunia na kusisitiza kuwa yeye kama Rais yupo bega kwa bega na timu hiyo ambapo ameitaka Wizara kuwaibua makocha wengine wa kike na kiume na kuwapatia mafunzo ili wawe wa kimataifa watakaosaidia kuinua kiwango cha soka nchini.
Amesema kutokana na kufanya vizuri kwenye michezo, mataifa makubwa duniani yameanza kufuatilia wachezaji nchini.
“Macho ya Timu kubwa wanafuatilia dumisheni nidhamu” amesisitiza Mhe Rais
Kwa upande mwingine Mhe. Rais amesema anatambua taasisi za Wizara kama BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu zina bajeti ndogo ambapo amesema baada ya miezi sita zitakwenda kupitiwa na kuelekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukaa na Wizara ya Fedha kupeleka hoja na amesisitiza kuwa atasaidia suala hili ili zipatiwe bajeti ya kutosha ziweze kufanya vizuri.
“Naomba Wizara mkae na Wizara ya Fedha mjieleze vizuri nami nitaweka nguvu huko”. Amefafanua Mhe.Rais Samia
Ameitaka Wizara kuwa wabunifu na kuvutia vijana katika michezo ili kuwandaa kwenye ajira ambapo ameagiza kupata mrejesho wa suala hili katika miezi mitatu ijayo.
Ameitaka pia Wizara kuangalia na kujadili vyanzo vipya vya fedha kufadhili Sanaa, Utamaduni na Michezo ambapo ametaka kuangalia maeneo ya kuwapunguzia tozo na kodi wasanii na wanamichezo pia kuwapa vivutio vya kikodi ili wawekezaji waweze kuwekeza kwenye maeneo hayo.
Kwa upande mwingine ameitaka Wizara kuja na mpango madhubuti wa kufadhili mchezo wa soka kwa wanaume na wanawake na ameitaka Wizara ya Utamaduni kushirikiana na TAMISEMI kuibua vipaji katika michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA na kuvikuza.
Amefafanua kuwa wanamichezo wana nafasi kubwa ya kutambulisha utalii wa nchi yetu duniani.
Akizungumzia kuhusu Muundo wa Wizara amesema amefanya mabadiliko ya Wizara kwa kuiondoa Idara ya Habari kuipeleka mahali inakohusika ili viongozi wa Wizara wajielekeze zaidi kwenye sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Amewapongeza Mawaziri kwa kuaminiwa na kuendelea kutumikia kwenye nafasi zao na kuwataka kwenda kushirikiana na kuchapa kazi siyo kugombana.
Ameeleza kuwa sekta za utamaduni, Sanaa na Michezo ni sekta za kipaombele ambazo pia zimeainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020-2025 na zinatoa ajira kwa wananchi.