Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameelezea aibu iliyolikumba kanisa hilo pamoja na yeye mwenyewe kutokana na kiwango cha unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto uliofanywa na kanisa nchini Ufaransa.
Matamshi hayo ameyatoa mjini Vatican katika mahubiri yake ya kila Jumatano kwa waumini ambapo amezungumzia takriban watoto 330,000 wa Ufaransa ambao walinyanyaswa na mapadri na viongozi wengine wa kanisa hilo kuanzia miaka ya 1950.
Amesema idadi hiyo ni kubwa na kwamba anaelezea masikitiko yake na mateso ya kiwewe ambayo wahanga hao wamekuwa nayo. Papa Francis amewataka maaskofu wote na viongozi wa kidini kuchukua hatua zote muhimu ili kuzuia vitendo kama hivyo visijirudie tena.
Aidha, papa pia amewataka Wakatoliki wa Ufaransa kuhakikisha kwamba kanisa linabaki kuwa nyumba salama kwa wote.