Mkuu wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni, Papa Francis, ameelezea masikitiko yake makubwa kwa wahanga wa dhuluma za kingono uliotendwa na uongozi wa kanisa hilo nchini Ufaransa, baada ya kuchapishwa ripoti ya uchunguzi wa matukio hayo.
Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni, amesema kiongozi huyo amehuzunishwa sana na matokeo ya uchunguzi huo huru, ambao umegunduwa kuwa viongozi wa kanisa lake waliwanyanyasa kingono jumla ya watoto 216,000 ndani ya kipindi cha miongo saba, kuanzia mwaka 1950, na kisha wakaufunika uovu huo, kwa kile alichokiita "veli la ukimya".
Bruni amesema Papa Francis anawalilia kwanza wahanga kwa majeraha yao na anawashukuru kwa ujasiri wa kujitokeza hadharani kuzungumzia jaala yao.
Kwa upande mwengine, Papa Francis amelipongeza Kanisa Katoliki nchini Ufaransa kwa kuthubutu kuyachunguza na kuyaweka hadharani madhila hayo, huku akilitolea wito kuchukuwa hatua za haraka za fidia na uponyaji.