Tume imepokea barua kutoka kwa Mhe. Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiitaarifu Tume kuwepo kwa nafasi wazi ya Ubunge katika Jimbo la Ngorongoro, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Mkoani Arusha. Nafasi hiyo ilitokana na kufariki kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Mheshimiwa William Tate Ole Nasha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 27 Septemba, 2021. Mheshimiwa Spika ametoa taarifa hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya  Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343.

Vilevile, Tume imepokea barua kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, akiitaarifu Tume juu ya uwepo wa nafasi wazi ya Diwani katika kata ya Naumbu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara kufuatatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo Mhe. Rashidi Julius Aderehemani wa Chama cha Wananchi (CUF) kilichotokea tarehe 29 Agosti, 2021.

Kwa kuzingatia masharti ya Kifungu 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 13 (3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume imeandaa Uchaguzi Mdogo ili kujaza nafasi ya Ubunge Jimbo la Ngorongoro na nafasi za Udiwani kwenye Kata moja Tanzania Bara. Ratiba ya Uchaguzi huo Mdogo ni kama ifuatavyo: