Viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani wameahidi kupunguza viwango vya gesi ya kaboni inayochafua mazingira ,wakati wa mkutano wa kilele wa siku mbili ambao utaweka msingi wa kongamano la Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya tabia nchi mjini Glasgow, Scotland.

Kwa mujibu wa taarifa, viongozi hao wa kundi la G20 pia wamekubaliana kusitisha ufadhili wa miradi ya uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe japo hawakuweka muda wa mwisho wa kuondokana na utegemezi wa nishati ya makaa ya mawe kwenye nchi zao, hatua hiyo ikiwa ahueni kwa China na India zinazotumia nishati ya makaa ya mawe.

Uingereza ilitaraji kuwepo kwa ahadi thabiti za kufikisha mwisho matumizi ya nishati ya makaa ya mawe kuelekea mkutano wa Glasgow.

Kundi la G20 linawakilisha zaidi ya robo tatu ya nchi zinazoongoza kwa kutoa gesi chafu duniani, wakati mwenyeji wa mkutano huo Italia ikitarajia kuwepo kwa malengo thabiti ya jinsi ya kupunguza utoaji wa hewa ukaa pamoja na kuzisaidia nchi maskini kukabiliana na ongezeko la joto.

Waziri Mkuu wa Italia Mario Dradhi amewaambia viongozi kwenye mkutano huo wa mjini Rome kuwa wanahitaji kuweka malengo ya muda mrefu na mfupi ili kusaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.