Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Hashimu Juma Issa, (63) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka mawili, likiwemo la kuchapisha taarifa za uongo na kuzisambaza kwenye mtandao wa YouTube.

Mshtakiwa huyo amefikishwa Mahakamani hapo Alhamisi Oktoba 7, 2021 na kusomewa mashitaka hayo na Wakili wa Serikali Yusuph Abood mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu.

Wakili Abood alidai mahakamani kuwa Oktoba Mosi katika eneo la Kinondoni B, mtaa wa Ufipa, mshtakiwa alisambaza taarifa kwa lengo la kumchafua na kumdhalilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro.

Alidai kuwa mshtakiwa alichapisha kwenye kompyuta na kusambaza taarifa kuwa "Sirro ni gaidi namba moja nchini Tanzania na fisadi."

Ilidaiwa katika shitaka lingine kuwa Oktoba Mosi katika eneo la Kinondoni B, mtaa wa Ufipa, mshtakiwa alitoa maneno ya uchochezi  kuwa "Sirro ni gaidi namba moja nchini Tanzania na fisadi" kwa lengo la kutengeneza chuki kwa wananchi.

Mshitakiwa huyo alikana mashtaka hayo.Wakili  Abood amedai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika na uko katika hatua za mwisho.

Issa aliachiwa kwa dhamana baada ya kutakiwa kuwa na waadahamini wawili watakaosaini bondi ya Sh3 milioni kila mmoja, barua ya utambulisho pamoja na kitambulisho cha taifa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 28, 2021 itakapotajwa tena.

 

Credit:M,wananchi