Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limebaini mbinu mpya ya kusafirisha dawa za kulevya, maarufu unga, wahusika wakidaiwa kutumia njia ya vifungashio kwa kuchana kurasa za vitabu kisha kugandisha upya kwa kutumia gundi na kuweka dawa katikati ya kurasa mbili.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, alibainisha hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumkamata Dorin Finan Lawrance, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, akidaiwa kusafirisha dawa ya Heroine gram 728.5 kwenda nchi jirani.
Alidai kuwa mtuhumiwa alifika katika ofisi za kampuni ya usafirishaji ya DHL eneo la stendi ya zamani mjini Singida, akiwa ameongozana na mpenzi wake, raia wa Kenya, lakini baadaye mpenzi wake huyo alikimbia baada ya kubaini hatari ya kukamatwa.
Mutabihirwa alifafanua kuwa njia hiyo mpya siyo rahisi kuibaini kwa jinsi dawa hizo zinavyohifadhiwa kwa ustadi mkubwa ndani ya kurasa za vitabu vitatu kutokana na kuchana kurasa, kisha dawa kufungwa ndani kwa utaalamu wa hali ya juu.
Kamanda Mutabihirwa alisema kabla ya kufikia hatua ya kuandika anuani, mmoja wa maofisa wa Kampuni ya DHL aliushtukia mzigo huo, hivyo akahitaji ufunguliwe kwanza kwa uhakiki zaidi na mvutano ulianza na mtuhumiwa mmoja wa kiume aliamua kukimbia.
Alisema msako mkali unaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo afikishwe kwenye vyombo vya sheria kujibu tuhuma dhidi yake.